Rais William Ruto amedai kuwa aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua alikuwa ametishia wabunge akitaka wampigie magoti la sivyo awatume nyumbani.
Rais alisema hii ilikuwa moja wapo ya sababu kuu zilizochochea wabunge kuazimia kumbandua Gachagua kutoka ofisini.
Alisema alijaribu kadri ya uwezo wake kumwokoa naibu wake dhidi ya kuondolewa madarakani na Wabunge.
Rais alisema kwamba alimpa Gachagua fursa mara mbili mara mbili ili kujikomboa kutoka kwa kile alichokiita 'migogoro midogomidogo'.
Ruto alidai Gachagua alikuwa akianzisha vita na Wabunge na viongozi wengine wa Ikulu.
"Nilijaribu, kumuokoa, walipomkataa Gachagua mara ya kwanza, nilimkubalia, walipojaribu kumshtaki mara ya pili nilimuokoa, je nilichaguliwa kutumikia mtu mmoja au Wakenya?" Ruto alisema.
Ruto alisema kuwa Wakenya ndio waamuzi wa jinsi viongozi wanavyofanya kazi na mamlaka yote yako mikononi mwa Wakenya.
Alisema kuwa viongozi hawafai kuangazia kushughulikia masuala yanayowahusu viongozi badala ya kuangazia maendeleo ya Wakenya.
Rais alikuwa akizungumza Jumatatu wakati wa mahojiano na wanahabari kutoka eneo la Mlima Kenya katika Ikulu Ndogo ya Sagana.
Gachagua alifurushwa na bunge la kitaifa Oktoba mwaka 2024 na kuwa naibu wa kwanza wa rais kuondolewa ofisini na bunge katika historia ya Kenya.
Jumla ya wabunge 281 walipiga kura kuunga mkono hoja ya kuondolewa madarakani dhidi ya 44 waliopiga kura kumuokoa.
Rais alisema kuondolewa afisini kwa Gachagua ni uamuzi uliotolewa na wanasiasa kutoka eneo la Mlima Kenya.
“Waliomuondoa walifuata sheria, sikuwahi kutia saini popote kwamba aondolewe afisini,” Ruto alisema.
"Mimi ndiye niliyemteua Gachagua kwa mujibu wa katiba. Hata nilipomteua, niliwaomba viongozi kutoka Mlima Kenya wanisaidie mmoja wao awe mgombea mwenza wangu."