Rais William Ruto ameendeleza mashambulii dhidi ya aliyekuwa waziri wa utumishi wa umma Justin Muturi.
Rais alitetea hatua ya kumtimua aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi wakati wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.
Akizungumza katika kikao cha wanahabari katika eneo la Sagana State Lodge Jumatatu jioni, Ruto alidai kuwa Muturi alikuwa na upungufu katika utekelezaji wa majukumu yake kama Mwanasheria Mkuu.
Alisema alipomfanya Muturi kuwa mwanasheria mkuu (Muturi) alijieleza akisema huenda asingeweza kutekeleza jukumu hilo ipasavyo ikizingatiwa kwamba hajakuwa katika kazi ya uanasheria kwa muda mrefu tangu alipohudumu kama hakimu, mbunge na spika.
"Alisema huenda akazidiwa. Ni kosa langu kwa sababu nilimshawishi lakini ni kweli baada ya muda fulani niliona amezidiwa, ndiyo maana niliamua kumbadilisha na kumpa kazi ya kuwa waziri," Ruto alisema.
"Katikati aligoma kuja kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri, wewe ni waziri, lakini umegoma, nilipaswa kufanya nini?" Rais alisema.
Ruto alisema yeye ni mtu anayeamini katika kuwapa watu fursa ya pili, akiongeza kuwa watu wengi wanaopewa nafasi ya pili huwa wanajikomboa.
"Mimi ni mtu ninayeamini katika fursa za pili. Hata ilipokuwa vigumu kwake (Muturi) kuhudumu kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini kwa sababu alikuwa rafiki yangu, tuliyefanya kazi pamoja, tuliyefanya kampeni pamoja, nilikuwa tayari kumpa fursa ya pili," Rais alisema.
"Nilimpa rafiki yangu mzuri Muturi nafasi ya pili, lakini katika mchakato huo, alijiondoa. Unatarajia nifanye nini?” Ruto alikariri.
Justin Muturi alionekana kutofautina na Rais Ruto wakati mwanawe alipotekwa nyara na kisha kuachiliwa wakati wa maandamano ya GenZ mwaka jana.
Muturi alikashifu serikali kwa kuendeleza utekaji nyara wa vijana ambao walionekana kutofautiana na sera za serikali.