Taifa la Sudan lilisisitiza kuwa vikwazo vilivyowekwa vya kutonunua bidhaa kutoka taifa la Kenya vingali imara.
Katika barua yake rasmi ilioandikwa na ubalozi wake hapa nchini Kenya -Nairobi taifa hilo lilisisitiza kuwa marufuku iliyotolewa na taifa hilo ingali imara na haijabadili nia wala msimamo kwa hilo kamwe.
Barua hiyo iliyoandikwa ,mnamo Aprili 1,2025 iliweza kukanusha madai na fikra kuwa mazao kutoka taifa la Kenya yangali yanauzwa katika taifa la Sudan kwa kiwango kikubwa kama ilivyokuwa hapo awali.
''Ubalozi wa Sudan katika mji wa Nairobi ungependa kuweka mambo bayana kuhusu kanuni za biashara za bidhaa kutoka taifa la Kenya.'' Sehemu ya barua hiyo ilieleza.
Mnamo Machi 11,2025 wizara ya biashara ya taifa la Sudan iliweza kutoa amri ya kusitisha bidhaa zote zinazonunuliwa kutoka taifa la Kenya kutokana na masilahi ya binafsi ya taifa la Sudan.
''Maamuzi hayo yametekelezwa sawasawa na hakuna bidhaa zozote kutoka taifa la Kenya zimenunuliwa kufikia sasa'' aya katika barua hiyo iliendelea kueleza.
''Taifa la Sudan linasalia imara kwa kuimarisha kanuni zote kulingana na mujibu wake wa kidiplomasia wa biashara, na kusisitiza kuwa madai yoyote yanayosema kuwa biashara ya ununuzi wa bidhaa kutoka Kenya inaendelea ni habari za uongo na ambazo hazijadhibitishwa ipasavyo''.
Kwa wakati huo huo Sudan ilisisitiza kupitia kwa ubalozi wake kuwa iko huru na ina ari kuu katika ukanda wa mataifa jumuishi katika mdahalo ambao unaazimia kuleta umoja, ushirikiano na utangamano kulingana na masharti ya utunzi wa kanuni zake kwa manufaa ya mataifa yote kwa heshima pasi mwingiliano wowote maelezo kutoka kwa barua yalifafanua.
Barua hiyo ya Ubalozi wa Sudani iliandikwa siku moja tu baada ya Rais William Ruto alipokuwa katika mahojiano na waandishi wa Habari mnamo tarehe 31 Machi ,2025 alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu hali na ushirikiano wa kidiplomasia na biashara kuhusu taifa la Kenya na Sudan.
Katika Jawabu lake Rais Ruto alisema kuwa Kenya ilikuwa ikiendelea kuuza bidhaa zake katika taifa hilo la Sudan pasi vikwazo vyovyote na kiwngo kikubwa kinachouzwa ni zao la Majani chai Rais Ruto alisema.
Marufuku ya Kibiashara kati ya Taifa la Sudan na Kenya ilitolewa na Sudan baada ya Kenya kuwa Mwenyeji na kualika kundi haramu la Rapid Support Forces (RSF) linalopinga utawala wa sasa wa serikali ya Sudan.