
Wakenya wametahadharishwa kujiandaa kwa mvua zaidi itakayoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa muda wa siku saba zijazo, kulingana na utabiri mpya kutoka kwa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini.
Katika taarifa yake ya kila wiki, idara hiyo imeeleza kuwa kunatarajiwa vipindi vya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ya Nyanda za Juu Magharibi na Mashariki mwa Bonde la Ufa — ikiwemo Nairobi — pamoja na eneo la Ziwa Victoria, maeneo ya chini Kusini Mashariki, na Kaskazini Mashariki mwa nchi.
Katika Nyanda za Juu Magharibi, Bonde la Ufa, na eneo la Ziwa Victoria, kutakuwa na mvua nyepesi asubuhi katika maeneo machache, kisha vipindi vya jua. Hata hivyo, dhoruba na mvua za jioni zinatarajiwa katika maeneo mengi, huku mvua za usiku zikitarajiwa sehemu chache na wakati mwingine kusambaa zaidi.
Maeneo yatakayoathiriwa ni pamoja na kaunti za Nandi, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Siaya, Busia, Baringo, Nakuru, Trans-Nzoia, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Pokot Magharibi, Kisii, Nyamira, Kericho, Bomet, Kisumu, Homa Bay, Migori na Narok.
Kaskazini mwa nchi, kaunti za Turkana na Samburu zitakumbwa na mvua asubuhi, alasiri, na usiku.
Katika maeneo ya Nyanda za Juu za Kati na Mashariki — ikiwa ni pamoja na Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka-Nithi na Nairobi — kutakuwa na mawingu asubuhi na mvua nyepesi, na baadaye jioni na usiku kutarajiwa mvua na radi sehemu chache.
Kaskazini Mashariki, katika kaunti za Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa na Isiolo, mvua za asubuhi pamoja na mvua za jioni na usiku zitatokea katika maeneo machache.
Kaunti za Machakos, Kitui, Makueni, Kajiado, Taita-Taveta pamoja na maeneo ya bara ya Tana River zitakuwa na mawingu na mvua nyepesi asubuhi, kisha mvua na radi alasiri na usiku katika baadhi ya maeneo.
Pwani ya Kenya—ikiwemo Mombasa, Kilifi, Lamu, Kwale, na maeneo ya pwani ya Tana River—itatandikwa na mvua asubuhi, alasiri na usiku katika maeneo ya hapa na pale kwa wiki nzima.