Hakimu Monica Kivuti aliyepigwa risasi na polisi mahakamani ameaga dunia

Kivuti alifariki katika Hospitali ya Nairobi, alikokuwa amehamishiwa baada ya tukio hilo.

Muhtasari

•Chanzo cha familia na wafanyakazi wenzake, ambao hawakutaka kutajwa majina, walithibitisha kifo chake kwa Radio Jambo mnamo Ijumaa.

•Kivuti alipigwa risasi Alhamisi alasiri katika Mahakama ya Sheria ya Makadara baada ya kutoa uamuzi katika kesi inayomhusisha mke wa polisi.

Monica Kivuti
Image: HISANI

Hakimu Mkuu wa Makadara Monica Kivuti ameaga dunia. Alikufa kutokana na kisa cha kupigwa risasi kilichomhusisha afisa Mkuu wa Polisi siku ya Alhamisi.

Chanzo cha familia na wafanyakazi wenzake, ambao hawakutaka kutajwa majina, walithibitisha kifo chake kwa Radio Jambo mnamo Ijumaa.

Kivuti alifariki katika Hospitali ya Nairobi, alikokuwa amehamishiwa baada ya tukio hilo. Chanzo cha habari katika hospitali hiyo kiliripoti kuwa aliaga dunia saa tano usiku.

"Ini na utumbo wake ulipasuka kwa risasi," chanzo kilisema.

Familia hiyo ilisema mwili wake umehamishiwa kwenye Mochari ya Lee.

Hakimu Kivuti alikuwa amepigwa risasi mguuni na kifuani.

Hapo awali alikimbizwa katika Hospitali ya Metropolitan na baadaye kuhamishiwa Nairobi Hospital, ambako alifariki.

Siku ya Ijumaa, ombi la dharura la uchangiaji wa damu lilitolewa ili kuokoa maisha yake.

"Ombi la dharura la uchangiaji wa damu. Hii ni kuomba mchango wa damu kwa Mhe Monica Kivuti," alitangaza Omwanza Ombati, mwakilishi wa kiume wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) katika Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

Kivuti alipigwa risasi Alhamisi alasiri katika Mahakama ya Sheria ya Makadara baada ya kutoa uamuzi katika kesi inayomhusisha mke wa polisi.

Mahakama ilisema hakimu "amefuta dhamana kwa mshtakiwa ambaye aliruka dhamana na kushindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kwa kufanya hivyo."

"Mara baada ya uamuzi huu, mtu alimpiga risasi hakimu na kumjeruhi kwenye nyonga," ilisoma taarifa ya mahakama.

Mshambuliaji aliyetambulika kwa jina la Inspekta Mkuu Samson Kipchirchir Kipruto, ambaye alikuwa msimamizi wa kituo cha polisi cha Londiani, Kisumu, alichomoa bunduki na kumpiga hakimu na kumjeruhi.

Maafisa wengine mahakamani walijibu haraka, huku afisa mmoja akimpiga risasi na kumuua Kipruto.

Maafisa wengine watatu walijeruhiwa katika tukio hilo, kulingana na ripoti ya polisi.

Kipruto alikuwa amesafiri kutoka kituo chake cha Londiani kuhudhuria kesi mahakamani inayomhusisha mkewe Jennifer Wairimu, 48, ambaye alikuwa mgonjwa, ambaye alishtakiwa kwa kupata Sh2.9 milioni kwa njia za uwongo.

Wairimu alikuwa ameomba kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu, lakini hakimu alikanusha ombi hilo baada ya kutohudhuria vikao vya mahakama kwa sababu ya ugonjwa.

Hati ya kukamatwa kwake ilikuwa imetolewa.

Alipofika Alhamisi, Juni 13, dhamana yake ilighairiwa, na hakimu akaamuru azuiliwe katika Gereza la Wanawake la Lang'ata.

Hili lilimkasirisha Kipruto, ambaye aliingia kortini kwa siri kupitia mlango wa hakimu na kufyatua risasi na kumpiga Kivuti kifuani na nyonga ya kushoto.

Wenzake waliokuwepo walifyatua risasi na kumuua papo hapo.

Kufuatia ufyatuaji risasi huo, shughuli za mahakama zilisitishwa siku ya Ijumaa.

Mahakama imeanza ushauri nasaha wa kijamii na msaada kwa maafisa wa mahakama na wafanyikazi katika Mahakama za Sheria za Makadara.