Pwagu kapata pwaguzi! Jambazi apokonywa bunduki na mwanaume aliyemwibia Sh200

Muhtasari

•Jambazi huyo alipomvamia Irungu alielekeza bunduki yake kwenye kifua chake na kumwamuru alale chini bila kusita.

•Jambazi huyo alikuwa na bahati ya mtende kwa kuwa mhasiriwa hakuwa na ujuzi wa kutumia bunduki


Image: TWITTER// DCI

Jambazi aliyemvamia mwanaume katika eneo la Chaka, kaunti ya Nyeri aliponea kifo chupuchupu baada ya mhasiriwa wake kumlemea nguvu na kumnyang'anya bunduki usiku wa Jumanne. 

Mshukiwa alimvizia Irungu Mwangi, 55, karibu na Shule ya Msingi ya Chaka mwendo wa saa mbili usiku huku akiwa amejihami na bunduki aina ya AK-47.

Jambazi huyo alipomvamia Irungu alielekeza bunduki yake kwenye kifua chake na kumwamuru alale chini bila kusita.

Irungu alitii amri na kukabidhi mshukiwa noti ya Ksh200 aliyokuwa nayo mfukoni wakati aliagizwa kutoa pesa zake zote.

Jambazi huyo ambaye hakuridhishwa na kiasi cha pesa ambacho Irungu alimpatia alimwagiza kutoa pesa zaidi ila akasita. Hapo akaanza kupora mifuko yake akitumai kupata pesa zaidi.

Wakati jambazi alikuwa anaendelea kupora mifuko yake Irungu alipata nafasi ya kumwangusha na kuchukua bunduki yake.

Jambazi huyo alikuwa na bahati ya mtende kwa kuwa mhasiriwa hakuwa na ujuzi wa kutumia bunduki. Wakati Irungu alikuwa anajaribu kufyatua risasi mshukiwa alipata nafasi ya kutoroka na kutoweka.

Irungu alisema ujuzi wake wa kukabiliana na wahalifu ulitokana na kuishi karibu na Chuo cha mafunzo ya polisi cha Kiganjo ambapo amekuwa akiwachungulia makurutu wakipata mafunzo.

Kitengo cha DCI kimeripoti kuwa polisi waliweza kubaini kuwa bunduki hiyo  ambayo ilikuwa na risasi 15 ilikuwa imeibiwa kutoka kituo cha polisi cha Nairutia mnamo April 15, 2022.

Polisi pia waliweza kupata kofia ya polisi wa AP katika eneo la tukio. Msako mkali umeanzishwa dhidi ya mshukiwa.