Tanzia! Aliyekuwa msaidizi wa Dedan Kimathi, Field Marshall Muthoni aaga dunia

Muthoni alifariki akiwa na umri wa miaka 92.

Muhtasari

•Shujaa huyo ambaye alipigana pamoja na marehemu Dedan Kimathi Waciuri katika Mlima Kenya na misitu alikata roho siku ya Jumatatu usiku.

•Gachagua alibainisha kuwa daima Wakenya watakuwa na deni kwa wapigania uhuru kama vile Muthoni kwa juhudi zao kubwa za kuwatimua wakoloni.

pamoja na naibu rais Rigathi Gachagua.
Field Marshal Muthoni pamoja na naibu rais Rigathi Gachagua.
Image: HISANI

Mpigania uhuru mkongwe wa Kenya Field Marshall Muthoni Kirima amefariki dunia.

Shujaa huyo ambaye alipigana na wakoloni pamoja na marehemu Dedan Kimathi Waciuri katika Mlima Kenya na misitu ya Aberdare alikata roho siku ya Jumatatu usiku.

Naibu Rais Rigathi Gachagua amemuomboleza marehemu Muthoni na kumpongeza kwa ushujaa wake na mchango wake mkubwa katika uhuru wa nchi.

"Nimeamka na habari za kusikitisha za kufariki kwa Field Marshall Muthoni Kirima, mpigania uhuru shupavu ambaye alipigana bega kwa bega na Field Marshall Dedan Kimathi Wachiuri katika misitu ya Mlima Kenya na Aberdare kuwafukuza wakoloni katika ardhi yetu," Gachagua alisema katika taarifa siku ya Jumanne asubuhi.

Aliongeza, "Ninaungana na familia yake na vizazi vya Vita vya Ukombozi vya Mau Mau kuomboleza kifo cha Mama yetu Field Marshall Muthoni wa Kirima."

Gachagua alibainisha kuwa daima Wakenya watakuwa na deni kwa wapigania uhuru kama vile Muthoni kwa juhudi zao kubwa za kuwatimua wakoloni.

Naibu rais aidha aliiombea roho ya marehemu Muthoni ipumzike kwa amani.

"Tunakumbuka kwa fahari na upendo, ushujaa wake katika kuongoza jeshi la ardhi na uhuru baada ya kutekwa kwa shujaa wa uhuru Dedan Kimathi, ambaye alihumu kama msaidizi wake wa kibinafsi, baada ya kusalitiwa na Washiriki. Tunabaki kuwa na deni kwa mashujaa na mashujaa hawa wakubwa kwa mchango wao wa kuikomboa Ardhi yetu. Mungu ampumzishe kwa amani na awape nguvu familia yake iweze kustahimili msiba huo,” alisema.

Muthoni alifariki akiwa na umri wa miaka 92. Roho yake ipumzike kwa amani.