Mlinda lango wa timu ya taifa ya Kenya, Patrick Matasi anauguza majeraha katika hospitali ya Kapsabet baada ya kuhusika kwenye ajali ya kutishia katika barabara ya Kapsabet-Nakuru siku ya Jumanne.
Kipa huyo ambaye kwa sasa anachezea klabu ya soka ya St George nchini Ethiopia alikuwa ameandamana na familia yake wakielekea mjini Nairobi walipokumbana na ajali hiyo walipofika pande za Lessos kaunti ya Nandi.
Inaripotiwa kuwa gari lakibinafsi walilokuwa wameabiri lilipoteza mwelekeo na kuvingirika mara kadhaa baada ya gurudumu kupasuka.
Matasi pamoja na wanafamilia wengine wane waliokuwa kwenye gari hilo walikimbizwa katika hospitali ya Kapsabet kwa gari la kubebea wagonjwa.
Wote watano walinusurika ajali hiyo na majeraha kadhaa mwilini.