Mwanariadha Mark Otieno kutoka Kenya ambaye aliondolewa kwenye mashindano ya Olimpiki yanayoendelea jijini Tokyo, Japan kwa madai ya utumizi wa dawa za kusisimua misuli amesisitiza kuwa hana hatia.
Matokeo ya vipimo vya kidaktari yaliyoachiliwa na maabara yaliashiria kuwa sampuli ya mkojo aliyopatiana mwanariadha huyo mnamo Julai 28 ilionyesha dalilli za matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku.
Kupitia ujumbe alioandikia Walimwengu siku ya Jumamosi, Mark alidai kuwa hajawahi kujihusisha na matumizi ya dawa zozote haramu.
"Uadilifu wangu kama mwanariadha na mtu binafsi ni muhimu sana kwangu na naheshimu sana nafasi niliyopewa kuwakilisha taifa langu ulimwenguni kama nilivyofanya mara mingi hapo awali. Kufuatia hayo siwezi jihusisha na kitendo chochote ambacho kitaniweka kwenye hatari ama kuhatarisha wenzangu" Mark Alisema.
Mwanariadha huyo wa mbio za mita 100 alisema kuwa walikuwa wamekata rufaa kuhusiana na maamuzi hayo na kuomba kufanyika kwa vipimo vingine.
"Kuwakilisha nchi yangu kwenye Olimpiki ni ndoto ambayo nimekuwa nayo kwa miaka mingi na inasikitisha sana kuona kuwa ndoto hii na imani ambayo mashabiki wangu na taifa langu wameniwekea imekatizwa. Kuwakilisha Mungu ni muhimu sana kwangu na amekuwa mwema kwangu kufikia sasa. Naamini kuwa atanipeleka mbali. Bado nashikilia imani kuwa nitasafisha jina langu na kuendelea na safari yangu kwenye riadha" Alisema Mark Otieno.