logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Niko tayari kukosa mashindano yajayo mradi tu nisichanjwe - Djokovic

Novak Djokovic alisema kwamba yuko radhi kukosa mashindano ya tenisi ilmradi asipate chanjo ya Corona

image
na Davis Ojiambo

Michezo16 February 2022 - 03:23

Muhtasari


  • • Novak Djokovic ameibua madai mapya na kusisitiza msimamo wake kwamba yuko tayari kufanya lolote ikiwemo kukosa mashindano yajayo ya tenisi almradi asilazimishiwe kupata chanjo ya kirusi cha Corona.
  • • Djokovic alifungiwa nje kushiriki katika Australia Open baada ya Waziri wa uhamiaji Alex Hawkes kuingilia suala hilo na kufutilia mbali visa yake ya usafiri kuingia jijini Melbourne.
  • • Djokovic alisema kwamba yuko radhi kukosa kwa sababu kanuni za kufanya maamuzi juu ya mwili wake ni ya umuhimu mkuu kuliko taji lolote la mashindano hayo.

Mchezaji nguli wa tenisi, Novak Djokovic ameibua madai mapya na kusisitiza msimamo wake kwamba yuko tayari kufanya lolote ikiwemo kukosa mashindano yajayo ya tenisi almradi asilazimishiwe kupata chanjo ya kirusi cha Corona.

Mchezaji huyo ambaye ameshikilia rekodi ya kuwa mchezaji bora wa tenisi kote duniani kwa Zaidi ya wiki 360 alisema haya katika mahojiano ya shirika la BBC.

Haya yanakuja wiki chache baada ya kufungiwa nje kushiriki mashindano ya tenisi yaliyofanyika nchini Australia mwezi jana kwa madai ya kutochanjwa dhidi ya Corona.

Djokovic alifungiwa nje kushiriki katika Australia Open baada ya Waziri wa uhamiaji Alex Hawkes kuingilia suala hilo na kufutilia mbali visa yake ya usafiri kuingia jijini Melbourne.

Katika mahojiano hayo na BBC, Djokovic alisema kwamba hayuko kinyume na chanjo hiyo ila kunafaa kuwe na uhuru wa mtu kuchagua kitu ambacho kinaingia mwilini mwake.

Alipoulizwa ni kwa nini yuko tayari kukosa mashindano ya tenisi ya siku za mbeleni kwa sababu ya chanjo, Djokovic alisema kwamba yuko radhi kukosa kwa sababu kanuni za kufanya maamuzi juu ya mwili wake ni ya umuhimu mkuu kuliko taji lolote la mashindano hayo.

“Ninajaribu sana kuwa saw ana mwili wangu iwezekanavyo,” alisema Djokovic

Ila baadae mchezaji huyo alifichua kwamba huenda ataridhia kupokea chanjo hiyo siku za mbeleni ila isiwe ni kulazimishwa na ataridhia kuipokea kwa sababu watu wote wanazidi kutafuta njia mwafaka na kutokomeza janga hilo la Corona.

“Katu mimi sikuwa kinyume na chanjo ya Corona. Ninaelewa kwamba kila mtu kote duniani anapambana ili kulimaliza janga hili na kuhakikisha kwamba tunalitokomeza hivi karibuni,” alisema Djokovic

Baada ya kufungiwa kuingia nchini Australia, Djokovic anaeleza kwamba alielewa fika kwamba taifa hilo limekuwa katika masharti magumu ya kufungiwa tangu janga hilo lilipoanza na kusema kwamba anawahurumia sana watu wa taifa hilo.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved