Baada ya mabingwa mara mbili wa kombe la klabu bingwa barani Uropa, Chelsea kudhibitisha kumfuta kazi kocha Thomas Tuchel mchana wa Jumatano, sasa tayari vyanzo vya habari barani Uropa vimeripoti kwamba timu hiyo inawamezea mate baadhi ya makocha tajika ili kuvivaa viatu vya Mjerumani huyo.
Mtandao wa Bleacher Report Football kwenye ukurasa wake wa Twitter tayari umeripoti kwa kuachia orodha ya makocha ambao fununu zinasema uongozi wa timu hiyo umewafuata kuwapa kazi kama mkufunzi.
Kulingana na Bleacher, Chelsea tayari imewalenga makocha kama vile aliyekuwa mchezaji na kocha wa Real Madrid Mfaransa Zinedine Zidane, Mauricio Pochettinho ambaye alifutwa kazi na klabu ya PSG miezi michache iliyopita, Kocha wa sasa wa Brighton & Hoven, Graham Potter miongoni mwa wengine.
Makocha wengine ambao wametajwa na baadhi ya mashirika ya habari za kispoti barani Uropa ni pamoja na aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew ambaye kwa sasa hana kazi baada ya kuachia ngazi mwaka 2018 timu ya Ujerumani ilipovurunda kipute cha kombe la dunia Urusi, aliyekuwa kocha wa Barcelona Luis Enrique ambaye kwa sasa ndiye kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uhispania kuelekea kombe la dunia nchini Qatar.
Kocha Thomas Tuchel alifutwa kazi baada ya timu ya Chelsea kufungua kampeni za ubingwa wa ulaya kwa kipigo mikononi mwa malimbukeni kutoka Croatia, Dyanmo Zagreb.
Tuchel anaondoka Chelsea baada ya mwaka mmoja na miezi kadhaa ambapo katika kipindi hicho aliisaidia Chelsea kushinda kombe la klabu bingwa Uropa na pia kushindwa klabu bingwa duniani.
Licha ya klabu hiyo kuwekeza katika kununua mabeki ghali zaidi msimu huu, imejipata ikifungwa mechi karibia zote katika kampeni zote za msimu huu mpaka sasa.
Shabiki wa kandanda mnadhani ni mkufunzi yupi atachukua nafasi ya Tuchel?