Baada ya kikao cha mawaziri wa rais Ruto kuidhinisha kung’oa nanga kwa shughuli za ukarabati wa viwanja mbalimbali vitakavyoandaa mashindano ya AFCON 2027 humu nchini, waziri wa michezo Ababu Namwamba sasa amefichua kwamba shughuli hizo zitang’oa nanga mapema mwezi ujao.
Kwa mujibu wa taarifa kwenye runinga ya Citizen, viwanja vya Kasarani jijini Nairobi na Kipchoge Keino mjini Eldoret vitafungwa kuanzia Novemba mosi ili kupisha shughuli za ukarabati.
Viwanja hivyo ni miongoni mwa viwanja vilivyopendekezwa na Kenya kwa CAF wakati wa kutuma ombi la pamoja na Tanzania na Uganda kuandaa mashindano hayo makubwa ya soka Afrika mwaka 2027.
Namwamba alidhibitisha kwamba shughuli ya ukarabati wa viwanja hivyo itaendeshwa na jeshi la Kenya, KDF ha shughuli hiyo inatarajiwa kukamilika mwaka 2025.
Baada ya kufungwa kwa viwanja hivyo, timu ya taifa sasa italazimika kushiriki mecho za kimataifa katika viwanja vya Ulinzi Complex jijini Nairobi na Kirigiti katika kaunti ya Kiambu.
Huku viwanja hivyo vikifungwa, ujenzi wa uwanja mpya wa Talanta katika barabara ya Ngong jijini Nairobi unatarajiwa pia kuanza kabla ya mwaka huu kukamilika.