Ilikuwa ni kipindi cha kujivunia kwa nahodha wa timu ya taifa ya Harambee Stars, Michael Olunga wakati alipotumia ujuzi wake mdogo wa lugha ya Kijapani kuwasaidia wachezaji wenzake wa Al Duhail kuwasiliana na mwamuzi wa Japani ambaye alikuwa akielekeza mechi yao ya Ligi ya Mabingwa wa Asia dhidi ya Persepolis mnamo Jumanne jioni.
Mwamuzi Jumpei Lida ambaye ana asili ya Japan alikuwa amechaguliwa kuchezesha mchezo huo wa hatua ya 6 bora wa ACL uliochezwa kwenye Uwanja wa Azazi mjini Tehran, Iran.
Wakati mechi hiyo ikiendelea, wachezaji wa Al Duhail ambao wengi wao ni Waarabu walihitaji mwamuzi huyo kueleza uamuzi uliotolewa uwanjani lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kuelewana vizuri kutokana na tofauti ya lugha, ndipo mwanasoka huyo wa kimataifa wa Kenya alipoingilia kati na kusaidia katika kutatua tatizo hilo.
"Katika mechi ya jana ya ACL, mwamuzi alikuwa Mjapani, lakini kutokana na Kijapani nilichosoma kidogo, niliweza kuwasiliana kwa niaba ya wachezaji wenzangu," Michael Olunga alisema kwa fahari kwenye akaunti yake ya Twitter Jumatano asubuhi.
Aliambatanisha maelezo yake na picha yake akionekana kufanya mazungumzo na mwamuzi wa Japan huku wachezaji wenzake wakitazama na kusikiliza kwa kuchanganyikiwa.
Olunga hata hivyo hakukosa kukiri kuwa lugha yake ya Kijapani haikuwa nzuri kiasi kikubwa.
"Ilikuwa ya kuchekesha kwa sababu (lugha) ilivunjika," alisema.
Mwishoni mwa mechi hiyo, klabu ya Olunga iliweza kuondoka na pointi zote tatu baada ya kuwalaza washindani wao wa Iran 1-2.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Kenya mwenye umri wa miaka 30 amekuwa akicheza nchini Qatar kwa miaka mitatu iliyopita tangu aondoke kwenye klabu ya Japan, Kashiwa Reysol mwaka wa 2020. Alikuwa ameichezea klabu hiyo kwa takriban misimu mitatu tangu 2018 kabla ya kuondoka Japan na kuelekea Qatar.
Olunga pia aliwahi kucheza nchini Uhispania, Uchina na Uswidi baada ya kuondoka Kenya 2015 kutafuta nafasi nzuri zaidi nje.