Klabu ya soka ya Nottingham Forest imemteua Mhispania Nuno Espirito Santo kama kocha mkuu wa kuwaelekeza mbele, masaa machache tu baada ya kumtimua Steve Cooper.
Klabu hiyo ambayo kwa sasa inashika nafasi ya 17 kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza ilitangaza uteuzi wa Nuno Jumatano mchana kupitia tovuti yake rasmi.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 49 alisaini mkataba wa miaka miwili na nusu baada ya kujiunga na klabu hiyo na ataanza kutoa huduma yake mara moja.
"Nottingham Forest leo inaweza kuthibitisha uteuzi wa Nuno Espírito Santo kama kocha mkuu wa kikosi cha kwanza. Nuno anajiunga na klabu hiyo kwa kandarasi ya miaka miwili na nusu na atachukua usukani wa mechi yake ya kwanza Jumamosi wakati Forest watakapomenyana na Bournemouth katika uwanja wa The City Ground,” Nottingham alitangaza katika taarifa yake Jumatano.
Mhispania huyo mwenye uzoefu anarejea katika Ligi ya Premia takriban miaka miwili baada ya kutimuliwa na klabu ya Tottenham Hostspurs. Alikuwa ameiongoza klabu hiyo yenye maskani yake London kwa chini ya miezi mitano kabla ya kutimuliwa mnamo Novemba 2021 baada ya kuisimamia klabu hiyo katika mechi 17 pekee.
Kabla ya kujiunga na Spurs mapema mwaka wa 2021, Nuno alikuwa ameiongoza Wolverhampton Wanderers tangu 2017. Alikuwa kocha wa Wolves kwa misimu minne mfululizo na aliisaidia klabu hiyo kushinda taji la Ubingwa la Sky Bet na kuipeleka katika robo fainali ya ligi ya Europa msimu wa 2019/20.
Baadaye, Nuno aliteuliwa kuwa meneja wa klabu ya Saudi Arabia, Al-Ittihad mwezi Julai 2022 ambapo alishinda taji la ligi na Saudi Super Cup kabla ya kutimuliwa Novemba 2023.