Timu ya Police FC imevutia maoni kinzani katika mitandao ya kijamii baada ya kutangaza bei za tikiti za mechi yao ya ligi kuu ya FKF-PL dhidi ya Gor Mahia wikendi hii.
Mechi hiyo ya ligi ya FKF-PL itachezwa Jumamosi katika uwanja wa Police Sacco maeneo ya South C jijini Nairobi kuanzia majira ya saa tisa alasiri.
Kwa kawaida, mechi zinazohusisha miamba wa soka katika ligi ya nyumbani kama vile AFC Leopards, Gor Mahia na hata Shabana FC – timu zenye mashabiki wengi, tikiti huwa hazizidi shilingi 300, lakini Police FC ambao ni malimbukeni katika kandanda ya Kenya wametangaza tikiti za mechi zao zitakuwa zinauzwa kwa hadi shilingi elfu 3.
Kwa mujibu wa maelezo katika tovuti yao, Police FC walisema kwamba tikiti za rasharasha zitakuwa zinaenda kwa shilingi 1,500 huku zile za VIP zikiuzwa kwa shilingi 2,000 na VVIP zikiuzwa kwa shilingi 3,000.
Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wa Gor Mahia wametoa maoni yao wakihisi kwamba wanakomolewa na timu hiyo ya Police FC ambayo wanasema haina wingi wa mashabiki ikilinganishwa na upande wao.
Mashabiki hao wanasema Police FC inataka kutumia fursa ya wingi wa mashabiki wa Gor Mahia ili kuokota hela nyingi na wengine wanasema huenda hawatatokea kufuatilia mechi hiyo moja kwa moja uwanjani.
Haya hapa ni baadhi ya maoni kutoka kwa mashabiki na wapenzi wa soka katika ukurasa wao wa Facebook.
“Mkakati uliokusudiwa kuwazuia mashabiki wa Gor mahia kutoka uwanjani wakati huu mgumu wa kiuchumi. Soka inawahusu mashabiki,” North West Kisumu Times.
“Sii mngesema tuu mnataka behind closed doors nkt” Njoki Njeri alisema.
“Ingekuwa NI Kogalo wako Home tungelipa but Nyinyi ngooouuu,” Julius Mauya Okodo.