Baada ya Nigeria kufana katika kipute cha AFCON, Super Eagles wamevutia mashabiki wengi kutoka nje na ndani ya bara la Afrika wengi wao wakiwa wanasoka waliostaafu.
Rio Ferdinand, beki wa zamani wa Man Utd ni mmoja wa wale ambao wameonesha kusimama na Nigeria katika fainali ya Jumapili dhidi ya mwenyeji Cote D’Ivoire.
Hata hivyo, huwezi kuzungumzia ufanisi wa timu ya taifa ya Nigeria bila kumzungumzia mwamba Stanley Nwabali ambaye amekuwa akisimama vizuri michumani kuhakikisha hakuna bao Nigeria inafungwa.
Kufuatia ufanisi wake langoni, baadhi ya Wanigeria wametoa wito kwa Ferdinand kuishawishi Manchester United kumsajili Nwabali kama mlinda lango wao ili kumweka benchi kipa wa Cameroon Andre Onana ambaye mwanzo wake michumani umekuwa wa kutiliwa shaka mno.
Mshambulizi wa timu ya kina dada ya Nigeria Super Falcons Asisat Oshoala kupitia ukurasa wa X alitoa maoni kwenye picha ya Ferdinand akiwa ameshikilia jezi ya Nigeria na kumtaka kutumia ushawishi katika katika Man U kuhakikisha Nwabali anachukua nafasi ya Onana.
Kipa huyo anayekipiga Afrika Kusini aliokoa mara mbili Nigeria ilipoilaza Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti kuweka hai ndoto zao za kushinda AFCON ya nne.
Nwabali amekuwa akiibuka kidedea kwenye michuano hiyo, kwa kuambulia patupu nne kuelekea fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Wakati huo huo, mlinda mlango wa Manchester United, Andre Onana aliangushwa kwenye benchi baada ya kuruhusu mabao matatu kwenye mchezo dhidi ya Senegal, kama ilivyoripotiwa na.
Mshambuliaji huyo wa Cameroon amekosolewa vikali kufuatia uchezaji wake akiwa na Mashetani Wekundu tangu ajiunge na klabu hiyo akitokea Inter Milan katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.