logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Wachezaji 62 wa Cameroon, akiwemo mdogo zaidi katika Afcon waadhibiwa kwa kudanganya umri

Douala anadaiwa kuwa na umri wa miaka 17 tu, lakini hata sura yake inaashiria wazi kwamba ana umri mkubwa zaidi

image
na Samuel Maina

Michezo12 March 2024 - 06:05

Muhtasari


  • •Wachezaji 62 waliosimamishwa kazi wanashukiwa kwa udanganyifu wa utambulisho na kuficha umri wao halisi.
  • •Douala anadaiwa kuwa na umri wa miaka 17 tu, lakini hata sura yake inaashiria wazi kwamba ana umri mkubwa zaidi

SHIRIKISHO la Soka la Cameroon (FECAFOOT) limewafurusha kwa muda wachezaji 62 kwa udanganyifu wa umri, akiwemo aliyekuwa mchezaji mdogo zaidi katika kikosi chao cha AFCON 2023, Wilfred Nathan Douala.

Ripoti kutoka nchi hiyo ya Afrika Magharibi zinaonyesha kuwa wachezaji waliosimamishwa kazi wanashukiwa kwa udanganyifu wa utambulisho na kuficha umri wao halisi.

Orodha rasmi ilitolewa na FECAFOOT mwishoni mwa wiki iliyopita, na miongoni mwa wachezaji waliosimamishwa ni Nathan Wilfred Douala, kiungo wa kati kutoka Victoria United ambaye alijumuishwa katika kikosi cha Cameroon cha Kombe la Mataifa ya Afrika 2023.

Kulingana na pasipoti ya kiungo huyo wa kati, ana umri wa miaka 17 tu, lakini hata sura yake inaashiria wazi kwamba ana umri mkubwa zaidi.

FECAFOOT ilisema nahodha wa Victoria United alidanganya kuhusu umri wake, na kwa hivyo mchezaji huyo ameondolewa kwenye mechi za mchujo za Ligi ya Wasomi.

Licha ya kujumuishwa katika kikosi cha Cameroon cha Afcon 2023, Douala hata hivyo hakucheza mechi yoyote wakati wa michuano hiyo ya mapema mwaka huu.

Mashabiki wa kandanda kote ulimwenguni walikuwa tayari wanatilia shaka umri wa mchezaji huyo wakati wa dimba la Afcon lililochezwa mwezi Januari-Februari kwani alionekana mzee zaidi ya miaka 17 kama ilivyodaiwa.

Umri halisi wa Douala haujawekwa wazi, lakini anaungana na wachezaji wengine 61 ambao pia wamesimamishwa kucheza kwa kuficha umri wao.

Kati ya timu 19 kwenye ligi kuu nchini Cameroon, ni 4 pekee ambazo hazijapata mchezaji yeyote anayeshukiwa kwa udanganyifu wa utambulisho na kuficha umri wao halisi.

Vilabu vinavyohusika vina haki ya kutoa stakabadhi zinazohitajika na kukata rufaa dhidi ya adhabu ndani ya masaa 72.

Katika majira ya joto ya 2022, shirikisho la kandanda la Cameroon liliwaita wachezaji 44 kutoka vilabu vinane tofauti kwa ajili ya kusikiliza madai ya umri au utambulisho wa kudanganya, huku rais wa shirikisho Samuel Eto'o akiwa na nia ya kutokomeza tatizo hilo katika nchi hiyo ya Afrika ya kati.

Miezi sita baadaye, Januari 2023, kulikuwa na kashfa mpya baada ya wachezaji 21 wa kikosi chao cha Chini ya miaka 17 kusimamishwa kutokana na suala hilo.

Udanganyifu wa umri umekuwa tatizo la muda mrefu kwa soka la Afrika, huku mafanikio yao mengi ya kimataifa katika ngazi ya vijana yakiwa yamegubikwa na madai ya wachezaji waliozidi umri.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved