Watu sita wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya mwanasoka wa Afrika Kusini Luke Fleurs.
Nyota huyo wa Kaizer Chiefs mwenye umri wa miaka 24 alipigwa risasi na kufa katika tukio la utekaji nyara katika kituo cha mafuta mjini Johannesburg wiki iliyopita.
Katika taarifa, polisi walisema kuwa washukiwa hao sita walikamatwa huko Soweto Jumatano asubuhi.
Polisi wanasema wanaamini "washukiwa hao ni sehemu ya kundi ambalo linahusika na utekaji nyara" katika jimbo la Gauteng.
Wachunguzi bado wanawasaka washukiwa zaidi. Maafisa walisema walipata gari la mwanasoka huyo, ambalo lilikuwa limeibiwa baadhi ya vifaa siku ya Jumatatu.
Bw Fleurs alikuwa akisubiri kuhudumiwa katika kituo cha mafuta alipofikiwa na watu wasiojulikana wenye silaha, ambao wakamwamuru ashuke nje ya gari, mamlaka zilisema.