Bingwa wa ndondi Francis Ngannou yuko katika hali ya majonzi kufuatia kifo cha mwanawe mchanga Kobe aliyeaga dunia siku ya Jumamosi, Aprili 27.
Bondia huyo kutoka nchi ya Cameroon alifichua habari za kusikitisha kuhusu kifo cha mvulana huyo wa miezi kumi na sita katika taarifa ya kihisia siku ya Jumatatu jioni.
Huku akimuomboleza mtotohuyo wake, Ngannou alimtambua kama mshirika wake, na mwenzake akisema kuwa ni mapema mno kwake kufa.
"Ni ghafla sana kuondoka lakini bado amekwenda. Mvulana wangu mdogo, mshirika wangu, mwenzangu Kobe alijawa na maisha na furaha,” Ngannou aliomboleza kupitia akaunti yake ya mtandao wa Instagram.
Aliendelea kufunguka jinsi kifo cha mvulana huyo kilivyomuathiri akibainisha kuwa maisha yake yalikuwa bora zaidi alipokuwa hai.
"Sasa, amelala bila uhai. Niliita jina lake tena na tena lakini hajibu. Nilikuwa bora karibu naye na sasa sijui mimi ni nani. Maisha si ya haki kutupiga pale ambapo inauma zaidi,” alisema.
Bondia huyo mashuhuri wa Afrika alitoa wito kwa wafuasi wake kumsaidia kukabiliana na hali hiyo ya kusikitisha akibainisha kuwa hana wazo la jinsi ya kupambana na huzuni.
“Unawezaje kukabiliana na jambo kama hilo? Unawezaje kuishi nayo? Tafadhali nisaidie ikiwa una wazo kwa sababu sijui la kufanya na jinsi ya kukabiliana na hili, "alisema.
Mtoto wa Ngannou, Kobe alizaliwa mwezi Januari mwaka jana na kupoteza maisha mnamo Aprili 27, mwaka huu.
Chanzo cha kifo chake bado hakijajulikana.