Gor Mahia imefanikiwa kuhifadhi taji la ligi kuu ya shirikisho la soka la Kenya, FKF kwa mara ya 21.
Kogalo waliwapepeta Muhoroni Youth 3-0 Jumapili, na kuhakikisha wanahifadhi taji hilo zikiwa zimesalia mechi tatu msimu kukamilika.
Bonface Omondi,Benson Omalla na Austin Odhiambo walicheka na nyavu kila mmoja na kusaidia timu hio kwenye ushindi muhimu.
Kenya Police,walikuwa wapinzani wakubwa wa taji hilo ila kushindwa na Tusker siku ya Jumamosi kulimaanisha kwamba Gor Mahia ilihitaji pointi moja katika mechi zao nne za mwisho ili kutawazwa mabingwa.
Gor Mahia sasa wamefuzu kwa ligi ya Mabingwa ya CAF msimu ujao.Ikumbukwe msimu uliopita walishindwa kujiunga kwenye mashindano hayo baada ya kushindwa kutimiza masharti ya leseni ya klabu.
Aidha mkufunzi Jonathan McKinstry, ambaye anatazamiwa kuondoka mwishoni mwa msimu ameelezea kufurahishwa na wachezaji wake msimu huu.
McKinstry atajiunga na timu ya taifa ya Gambia kama kocha mkuu.
'Nimefurahishwa sana na ninajivunia wachezaji wangu,kabla ya mechi niliwaelezea waimarike zaidi ili kutwaa alama ...' Mckinstry alieleza katika mahojiano baada ya mechi.
Baada ya mechi hio,McKinstry ameratibiwa kuelekea nchini Gambia ili kuongoza taifa hilo kwenye mechi za kufuzu kwa kombe la dunia 2026.