Timu ya taifa ya wachezaji 7 tayari iko mjini Madrid kwa ajili ya wikendi ambapo watawania kufuzu kwa msururu wa raga wa dunia katika mji mkuu wa Uhispania.
Kocha wa Shujaa, Kevin Wambua, aliwataja Victor Onyala na Tony Omondi kuwa manahodha wenza katika kikosi cha wachezaji 13, ambacho kinajumuisha mchezaji wa Mwamba RFC, Brian Mutua.
Shujaa watakuwa katika kundi B ambapo watamenyana na Samoa, Chile na wenyeji Uhispania.Kocha Kelvin ‘Bling’ Wambua ataanza kampeni yake dhidi ya Samoa saa sita na dakika ishirini na tano mchana,Ijumaa kabla ya pambano lao dhidi ya wenyeji Uhispania saa 10:18 jioni siku hiyo hiyo.
Pambano lao la mwisho la mchezo huo ni dhidi ya Chile Jumamosi saa 8:18 usiku ambapo Shujaa wanatumai watakuwa wamejikatia tiketi ya kushiriki shindano hilo la kifahari. Mafanikio nchini Uhispania yatasaidia sana kuwapa morale baada ya kuonyeshwa vumbi kwenye mechi za mchujo za mwaka jana huko Twickenham, London ambapo walifungwa 12-5 na Canada katika fainali.
Kabla ya kuondoka kuelekea Madrid, Shujaa wamekuwa katika mazoezi ya wiki mbili huko Miramas,Ufaransa ambapo walitia nanga baada ya kampeni yao huko Munich. Timu nne kutoka kwa mchujo huu zitafuzu kwa HSBC SVNS ya 2025, inayotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu.
Kikosi kilichosafiri:
Vincent Onyala, Tony Omondi, Kevin Wekesa, John Okoth, Brian Tanga, George Ooro, Patrick Odongo, Samuel Asati, Herman Humwa, Nygel Amaitsa, Lamec Ambetsa, Chrisant Ojwang, Brian Mutua.