Usiku wa kuamkia siku ya Jumatatu ulikuwa na matukio mawili makubwa ya soka.
Fainali za shindano kubwa zaidi barani Ulaya, Euro, na michuano mikubwa kabisa ya Amerika, Copa America, zilichezwa katika nyakati tofauti.
Uhispania ilishinda taji la Euro 2024 kwa kuifunga England katika fainali zilizokuwa zikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi zilizochezwa kwenye uwanja wa Olympiastadion mjini Berlin, Ujerumani.
Mechi hiyo iliyochezwa saa nne usiku wa Jumapili ilimalizika kwa mabao 2-1 huku Uhispania ikinyakua ushindi huo dakika ya 86 kupitia kwa kiungo Mikel Oyarzabal.
England walikuwa wamerejea kwenye mechi baada ya kiungo wa Chelsea Cole Palmer kuingia uwanjani na kufunga bao la kusawazisha dakika ya 73.
Bao hilo lilikuwa limefuta bao la Nico Williams alilofunga katika dakika ya 47, lakini halikutosha kuzuia England kushindwa.
Katika fainali ya pili iliyochezwa mwendo wa saa kumi asubuhi, Argentina ilishinda 1-0 katika muda wa nyongeza baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika bila bao.
Mshambulizi wa Inter Milan Lautaro Martinez alifunga bao pekee katika mechi hiyo dakika za lala salama baada ya timu zote mbili kufanya majaribio kadhaa ya kufunga.
Mechi hiyo ilijawa na mvutano mkubwa huku Argentina na Colombia zikifanya majaribio mengi ya kufunga.