Fabrizio Romano ni jina maarufu katika ulimwengu wa soka,hasa kwa wale wanaofuatilia kwa karibu habari za usajili wa wachezaji.
Romano alizaliwa Naples [Napoli] huko Italia Februari 21,1993 na alihudhuria chuo cha Università Cattolica del Sacro Cuore huko Milan. Ana uwezo wa kuzungumza Kiingereza, Kihispania, na Kiitaliano.
Romano alianza kazi yake katika uandishi wa habari za soka mwaka wa 2009 akiwa bado katika shule ya upili.
Mwanahabari huyo aligunduliwa na Garth Crooks, mnamo 2010, wakati Crooks alikuwa akisimamia hafla ya ushirika huko Fiat, ambapo Romano alikuwa mfanyakazi.
Baada ya kuvutiwa na ujuzi wake kwenye maandishi huko Italia, Crooks alimtumia barua pepe mkurugenzi mkuu wa BBC Tim Davie, akipendekeza kwamba Romano apewe sehemu ya wageni kwenye safu maarufu ya 'Crook's Team of the Week' kama mwandishi.
Mafanikio yake yalikuja mwaka wa 2011 alipopokea taarifa za ndani kutoka kwa wakala wa Kiitaliano huko Barcelona kuhusu mchezaji chipukizi wa Barcelona Mauro Icardi.
Romano alijiunga na Sky Sport Italia mwaka wa 2012, ambapo alianzisha uhusiano mkubwa na vilabu, mawakala, na wasuluhishi kote Ulaya. Vile vile amefanya kazi na vyombo mbalimbali vya habari kama vile The Guardian na CBS Sports.
Romano anajulikana kwa msemo wake "Here we go!", unaotumiwa kuashiria uthibitisho wa mpango wa uhamisho.
Mwanahabari huyo, anachukuliwa kuwa mojawapo ya vyanzo vya kutegemewa katika uga wa uhamisho wa kandanda.
Uaminifu wake na ufuasi mkubwa wa mitandao ya kijamii umesababisha vilabu kadhaa vya soka kumhusisha katika video za matangazo ya wachezaji.
Fabrizio alipokea tuzo ya mwanahabari bora wa Kandanda katika Tuzo za Globe Soccer za 2022 na tuzo ya "Mwanahabari Bora wa Dijitali" katika toleo la 2023.