Kiungo wa kati wa Croatia Luka Modric ameongeza mkataba wa mwaka mmoja na Real Madrid ambao utamweka Bernabeu hadi 2025,huku klabu hio ikithibitisha kuwa atachukua unahodha.
Mshindi huyo wa Ballon d'Or mwenye umri wa miaka 38 mwaka 2018 alishinda taji la sita la Ligi ya mabingwa na pia taji la nne la LaLiga akiwa na Real msimu uliopita.
Mkataba wa awali wa Modric uliisha mwishoni mwa msimu wa 2023-24 lakini mcroatia huyo aliwaambia mashabiki kwamba atarejea msimu ujao walipokuwa wakisherehekea ushindi wao wa Ligi ya mabingwa ambao uliongeza rekodi ya Real hadi 15 za kombe la Ulaya.
Kufuatia kuondoka kwa nahodha wa zamani,Nacho Fernandez,Modric ametangazwa kama nahodha mpya wa Real Madrid huku akitarajia kuwaongoza makinda kama vile Endrick.
Hakuna mchezaji aliyeshinda mataji mengi akiwa na Real Madrid kuliko Modric, ambaye amebeba mataji 26 tangu alipojiunga na wababe hao wa Uhispania mwaka 2012.
Mchezaji huyo mkongwe alitarajiwa kustaafu, haswa baada ya mwenzake wa muda mrefu wa kiungo cha kati Toni Kroos, 34, kutangaza kustaafu mwishoni mwa msimu huu.
Modric pia hakuwa na mpango wa kutundika daruga zake kwenye hatua ya kimataifa licha ya Croatia kutolewa mapema kwenye michuano ya Ulaya iliyomalizika hivi karibuni, ambapo waliondolewa baada ya hatua ya makundi.
"Ningependa kuendelea kucheza milele lakini pengine itafika wakati nitalazimika kutundika buti zangu. Nitaendelea kucheza, lakini sijui kwa muda gani," alisema Modric, ambaye amecheza mechi 178. taifa lake la Croatia.