Mwanariadha Eliud Kipchoge amefichua baadhi ya changamoto anapotarajia kushinda taji lake la tatu la Olimpiki katika michezo ya Olimpiki ya Paris.
Kwenye mazungumzo na CGTN sport;Bingwa huyo mara tano wa Berlin Marathon alikiri kuwa mbio hizo hazitakuwa kazi rahisi.
Kipchoge alidai kuwa hali ya hewa mjini Paris huwa ni ya joto mwezi Agosti, hivyo kuwa changamoto katika harakati zake za kuwania tuzo ya juu.
" ... ni joto sana huko Paris mnamo Agosti na pili, kozi ni ya juu na ya chini na hiyo ni changamoto kubwa kwa kila mtu. Hata hivyo, sitaki kulalamika kwa sababu sote tutakuwa tukikimbia katika eneo moja na hali ya hewa ile ile,” Kipchoge alisema
Pia ana kumbukumbu tamu za Paris, kwani ilikuwa nafasi ya kwanza ambapo alishiriki kwenye jukwaa la kimataifa, akishiriki katika mashindano ya dunia ya 2003 ambapo alishinda medali ya dhahabu katika mbio za 5000m.
"Mwaka wa 2003 ulikuwa mwanzo wa maisha yangu katika mchezo na naweza kusema nina furaha kurudi huko na kushindana na kuonyesha ulimwengu ambapo maisha yangu yalianzia na kuonyesha maisha marefu na upendo wa michezo," aliongeza.
Vile vile ,atakuwa anaeka historia, akiwa mkenya wa kwanza kushiriki mara tano kwenye michezo ya Olimpiki.