Kocha wa klabu ya Mara Sugar inayoshiriki ligi kuu nchini Kenya Bonface Ambani amekashifu hatua ya waziri wa michezo Kipchumba Murkomen kuwazawidi wachezaji wa timu ya wavulana ya taifa ya Kenya wasiozidi umri wa miaka 20 kitita cha shilingi milioni 1.8.
Timu hiyo baada ya kulakiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKIA mnamo Jumatatu, waliandaliwa staftahi siku ya Jumanne katika jumba la Talanta kuwasherehekea kutokana na kufuzu mashindano ya AFCON yatakayoandaliwa nchini Afrika Kusini mwaka wa 2025.
Kulingana na Ambani, amemtaka waziri Murkomen kuwacha kufanya utani na vijana hao wa Rising Stars akistaajabia zawadi murwa wizara ya michezo inaweza wapa wachezaji hao ni shilingi milioni 1.8 pekee.
“Ikiwa watagawana shilingi hizo pamoja na benchi la kiufundi, hiyo ni chini ya 40K… hii serikali inaweza kufanya vyema Zaidi ys hii.” Alimaka Ambani kwenye ukurasa wake wa Meta.
Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars, alisikitikia kuwa baada ya wiki mbili ya vijana wa Rising Stars kuweka kambi nchini Tanzania kwa ajili ya bendera ya taifa, kitu cha pekee serikali ya Kenya inaweza kuwapa ni shilingi 40,000.
“Serikali inaweza fanya zaidi ya hii, ni nini mbaya na hawa maafisa wa serikali. Wiki mbili na Zaidi nje ya nchi, kitu pekee wavulana hawa wanapewa ni elfu 40.” Aliandika kocha Ambani.
Bonface Ambani amewataka maafisa katika wizara ya michezo kuwacha utani huo akisema kuwa wachezaji na benchi la kiufundi wanastahili mazuri zaidi ya walichopewa.