Nahodha wa zamani wa Harambee Stars Victor Wanyama ameeleza nia yake ya kucheza pamoja na Cristiano Ronaldo mara tu atakapoondoka rasmi katika klabu ya MLS ya CF Montreal.
Kuondoka kwa Wanyama kulithibitishwa na klabu siku ya Alhamisi, na hivyo kuhitimisha muda wake wa takriban miaka mitano katika klabu hiyo.
"Kucheza na mtu kama Cristiano ni jambo kubwa sana. Yeye ni mtu maarufu ambaye kila mtu angependa kuwa naye katika timu yake," Wanyama alisema katika mahojiano na vyombo vya habari.
Kiungo huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur na Southampton anahisi bado ana uwezo wa kuichezea moja ya timu bora zaidi duniani.
“Bado naamini naweza kucheza popote kwa misimu miwili kwenye kiwango cha juu halafu labda niendelee na ligi za chini. Nimekuwa kila mahali sasa, kusema kweli, niko tayari kujaribu ligi zingine kama Uturuki, Saudi na ligi za Asia au labda kusalia MLS,” aliongeza.
Wanyama alikuwa miongoni mwa wachezaji wanane ambao Montreal iliamua kutoongeza muda.
Klabu hiyo ya Kanada ilikuwa ikimlipa mshahara mmkubwa wa shilingi milioni 233 kila mwaka.
Wanyama alikuwa mchezaji anayelipwa zaidi Montreal, na kuondoka kwake kutaipa klabu pesa zaidi kuleta jina lingine ili kusuluhisha.
Alicheza mechi 133 akifunga mabao sita katika mashindano yote akiwa na CF Montreal na alishinda Ubingwa wa Canada mnamo 2021.