Kenya Police FC iliendeleza msururu wa kutoshinda katika Ligi Kuu ya Kenya baada ya kulazimishwa sare tasa na Kariobangi Sharks katika uwanja wa Dandora mnamo Ijumaa.
Kocha mkuu wa Harambee Starlets Beldine Odemba aliongoza Polisi katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani wa kutosha baada ya timu hiyo kutimua benchi nzima ya kiufundi mnamo Alhamisi.
Afisa Mkuu Mtendaji wa klabu hiyo Chris Onguso alikuwa ameonya kuhusu hali tete baada ya kutoridhishwa na uchezaji duni uliojumuisha sare ya 1-1 dhidi ya Sofapaka na kufungwa 1-0 na Shabana.
Licha ya kushindwa kuiongoza timu hiyo kupata ushindi dhidi ya Kariobangi Sharks mnamo Ijumaa, Odemba aliandikisha historia kwa kuwa kocha wa pili wa kike kusimamia klabu ya ligi kuu ya wanaume.
Odemba kwa sasa ni kocha mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya, Police Bullets. Inabakia kuonekana kama, atajumuishwa katika benchi ya kiufundi ya wanaume kwa misingi ya kudumu.
Jackline Juma alikua mwanamke wa kwanza kufundisha timu katika daraja la juu la wanaume baada ya kuteuliwa kuwa kocha mkuu wa FC Talanta mwanzoni mwa msimu.
Alishinda mchezo wake wa kwanza akiwa mkufunzi, baada ya kuiongoza Talanta kushinda 1-0 dhidi ya Sofapaka kwenye Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos.
Matokeo hayo hayakuwasaidia Sharks pia kwani timu hiyo sasa imecheza mechi tano bila kushangilia ushindi.
Sharks ilishinda mechi ya ligi mara ya mwisho Septemba ilipoilaza Kakamega Homeboyz 1-0 uwanjani Mumias Sports Complex.
Klabu hiyo imesajili sare nne na kupoteza katika mechi tano zilizopita na itatafuta kurekebisha itakapomenyana na Bandari katika mchezo ujao.