MOHAMED SALAH ameweka shinikizo kwa Liverpool kumpa mkataba
mpya, akisema "kwa sasa anahisi yuko zaidi katika kuondoka kuliko
kusalia".
Salah, 32, alifichua kuwa bado hajapewa kandarasi mpya, huku
mkataba wake wa sasa ukikamilika msimu wa joto.
Salah alifunga mabao mawili dhidi ya Southampton Jumapili na
kuifanya Liverpool kuwa mbele kwa pointi nane kileleni mwa jedwali kabla ya
kufichua masikitiko yake ya kutopewa ofa.
Alisema: "Sawa, tunakaribia mwezi wa Desemba na
sijapokea ofa yoyote ya kusalia kwenye klabu. Pengine niko nje zaidi kuliko
ndani.”
"Sitastaafu hivi karibuni kwa hivyo ninacheza tu,
nikizingatia msimu na ninajaribu kushinda Ligi Kuu na ninatumai Ligi ya
Mabingwa pia.”
"Nimekata tamaa lakini tutaona."
Salah aliongeza: "Nawapenda mashabiki, mashabiki
wananipenda, mwisho haiko mikononi mwangu au mikononi mwa mashabiki, tusubiri
tuone.
"Unajua nimekuwa katika klabu kwa miaka mingi, hakuna
klabu kama hii. Lakini mwishowe, hatima haiko mikononi mwangu. Ni Desemba na
sijapokea chochote kuhusu mustakabali wangu."
Kuna hamu kubwa ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri
kutoka Saudi Pro League, huku Liverpool wakiwa wamekataa ofa za hadi pauni
milioni 150 hapo awali.
Alipoulizwa kuhusu matarajio ya kuhamia Mashariki ya Kati,
alisema: "Sitaki kuzungumza juu ya hilo.
"Ninalenga na timu sasa. Mimi ni mtaalamu sana. Kila
mtu anaweza kuona maadili yangu ya kazi. Najaribu tu kufurahia soka langu na
nitacheza katika kiwango cha juu kwa muda mrefu iwezekanavyo.”
"Ninafanya kila niwezalo kwa sababu hivi ndivyo nilivyo
na ninajaribu kutoa yote kwa ajili yangu na kwa ajili ya klabu. Tutaona
kitakachofuata."
Salah ni mmoja wa wachezaji watatu muhimu ambao kandarasi
yao itamalizika Anfield msimu wa joto, pamoja na Virgil van Dijk na Trent
Alexander-Arnold.
Van Dijk alifichua hivi majuzi kwamba mazungumzo yameanza
kuhusu kandarasi mpya, wakati Alexander-Arnold amenyamaza kabla ya Real Madrid
- ambao watatembelea Merseyside katika Ligi ya Mabingwa wiki hii.
Salah ana mabao 223 na asisti 99 katika mechi 367
alizoichezea Liverpool.