WABABE wa soka kutoka Misri, Al Ahly wamejitokeza
kunyoosha maelezo kuhusu tetesi zinazoenezwa mitandaoni kwamba wamo katika safu
ya vilabu vinavyowinda huduma za Cristiano Ronaldo.
Mreno huyo mwenye umri wa miaka 39 amekuwa
akihusishwa na kuondoka Al Nassr ya Saudi Arabia mwishoni mwa msimu huu huku
vilabu kadhaa vikitajwa kuwa katika mbio za kuwania saini yake.
Mkataba wa Ronaldo na Al Nassr unatarajiwa kukamilika
mwishoni mwa msimu na yupo huru kufanya mazungumzo ya kujiunga na klabu yoyote
kuanzia mwezi Janauri iwapo Al Nassr hawatampa mkataba mpya.
Moja ya vilabu ambavyo vimetajwa wiki hii ni Al Ahly
kutoka Misri ambao wamesemekana kuwa katika harakati za kuimarisha kikosi chao
kwa ajili ya michuano ya mwisho wa msimu – FIFA Club World Cup kati ya Juni na
Julai mwakani.
Klabu hiyo kutoka Cairo iko katika kundi A na Inter
Miami yake Lionel Messi, Porto, na Palmeiras.
Hata hivyo, uwezekano wa Ronaldo kuelekea Misri
unabaki na nafasi finyu baada ya ripoti kutoka klabuni kuibuka kwamba Al Ahly
hawako na mpango wa kumsajili Ronaldo.
Kwa mujibu wa Koora, chanzo kilicho karibu na uongozi
wa klabu hiyo, Al Ahly hawako tayari kufukuzia saini ya Ronaldo kutokana na
gharama kubwa ya mchezaji huyo maarufu kote duniani.
“Klabu
yoyote itataka kumsajili Ronaldo kwa sababu ni nguli wa soka na maarufu katika
hilo, lakini jina lake halikuwa miongoni mwa majina ambayo tuliwasilisha katika
meza ya majadiliano ya Al Ahly kwa sababu maelezo ya mkataba na malipo ya
mchezaji huyo yapo juu sana,’ chanzo kilisema.
“Ronaldo
anapokea mshahara mkubwa na Al Nassr ambao ni mkubwa kuzidi bajeti nzima ya
klabu ya Al Ahly,” ripoti hiyo iliongeza.
Ripoti hizi zinachipuka wakati ambapo kuna uvumi
kwamba Ronaldo yuko tayari kushiriki katika michuano ya FIFA Club World Cup,
baada ya klabu yake ya Al Nassr kufeli kujishikia nafasi.