
Mshambulizi wa zamani wa Brazil Ronaldo atawania kiti cha urais wa shirikisho la soka nchini humo (CBF), mchezaji huyo sasa ana umri wa miaka 48.
Ronaldo, ambaye alishinda Kombe la Dunia akiwa na Brazil mwaka 1994 na 2002, atagombea kama mgombea katika uchaguzi wa CBF ili kuchukua nafasi ya rais wa sasa Ednaldo Rodrigues katika mwaka wa 2026.
Ronaldo alisema kuwa anasumbuliwa na hali ya watu wengi wa nchi hiyo ya Brazil ambao sasa hawana upendo kwa timu hiyo ya Taifa.
‘’Miongoni mwa mamia ya mambo yanayonitia moyo kuwa mgombea urais wa CBF ni kurejesha umaarufu na heshima ambayo timu hii ya taifa imekuwa nayo siku zote na ambayo hakuna mtu mwingine aliye nayo leo.” Alisema Ronaldo.
Brazil wameshinda Copa America mara moja tangu Ronaldo alipostaafu katika michezo za kimataifa mwaka wa 2011 na kutolewa nje ya Kombe la Dunia la 2022 na Croatia katika robo fainali.
Nyota huyo wa kitambo aligadhabishwa na matokeo mabaya ya timu hiyo ya brazil licha ya kuwa na baadhi ya wachezaji bora zaidi ikiwemo Vinicius Junior, Estevao na Endrick.
‘’Tuna wachezaji bora, tuna Vinicius Junior, Neymar, Rodrygo, Estevao na Endrick miongoni mwa wengine wengi, tuna vipaji vingi, tunawezaje kutocheza vizuri tukiwa na hawa wote,’’ Alisema Ronaldo.
Mshambulizi huyo wa zamani wa Barcelona, Inter Milan na Real Madrid kwa sasa pia alisema anatarajia kuuza dau lake katika klabu inayoshiriki ligi kuu ya Uhispania Real Valladolid.
‘’Tunafanya mazungumzo ya uwezekano wa kuuza hivi karibuni na tunapaswa kufunga mpango huo. Haitakuwa kikwazo kwa ugombea wangu," Alisema nyota huyo.
Muhula wa Rodrigues utaendelea hadi Machi 2026 na uchaguzi wa urais lazima ufanyike katika miezi 12 kabla ya wakati huo.