
Ousmane Dembele alifunga bao la ushindi katika dakika za lala salama wakati Paris Saint-Germain iliishinda Monaco na kunyakua taji lake 13 la Trophee des Champions ikiwa ni rekodi kwa kutwaa taji hilo mara tatu mfululizo.
Kikosi cha Luis Enrique, kikisaidiwa na umati mkubwa wa mashabiki kwenye Uwanja wa 974, kilidhibiti sehemu kubwa ya mchezo huo lakini Monaco walikaribia kulazimisha penalti kabla ya bao lake Dembele katika dakika ya pili kati ya nne za muda ulioongezwa.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa alipokea pasi kutoka kwa Fabian Ruiz na kupata bao kutoka upande wa kulia wa eneo la yadi sita, na kupata ushindi uliostahili kwa PSG. PSG walikuwa na umilisi mkubwa wa mpira muda wote, wakikusanya mashuti 10 yaliyolenga lango - mara mbili ya jumla ya wapinzani wao.
Monaco waliimarika baada ya mapumziko na kugonga nguzo kupitia kwa Eliesse Ben Seghir na beki wa Brazil Vanderson.
Ingawa Köhn alifanya kazi nzuri ya kumnyima Achraf Hakimi nafasi katika dakika ya 74, alishindwa kusoma vyema krosi ya Ruiz na Monaco wakakosa kushinda kombe hilo kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2000.
PSG ilishinda kombe hilo, ambalo pia linajulikana kama Super Cup, kwa mara ya tatu mfululizo na kuongeza rekodi ya kuhifadhi kombe hilo mara 13 kwa jumla. PSG walishinda ligi na vikombe mara mbili msimu uliopita, huku Monaco wakimaliza ligi wakiwa nafasi ya pili.
Hata hivyo, kikosi cha Luis Enrique kilistahili ushindi huo na kupata kombe hilo sawa na ngao ya Jamii ya Uingereza maarufu kama community shield kwa mara ya 11 kati ya misimu 12 iliyopita, na hivyo kuzidisha ubabe wao wa ndani.
"Ilikuwa mechi ya kupendeza kati ya pande mbili kuonyesha kandanda bora, Matokeo ni taswira ya haki ya udhibiti wetu... dhidi ya moja ya timu bora nchini Ufaransa na Ulaya," Alisema Enrique.
Hapo awali mchuano huo ilipangwa kufanyika Beijing mnamo Agosti 8 kama utangulizi wa msimu wa Ufaransa,hata hivyo mechi hiyo ilihamishiwa hadi Doha baada ya mamlaka ya Uchina kufuta mechi hiyo.
Mchezo huo uliandaliwa kwenye Uwanja wa 974, uwanja ulioandaa fainali ya Kombe la Dunia ya 2022, ingawa hakukuwa na idadi ya mashabiki wa kujaza uwanja huo.