
Nafasi ya Ruben Amorim huko Manchester United tayari inaangaliwa upya, kulingana na ripoti.
Mashabiki wa United walifurahi kumuona Erik ten Hag akiondoka baada ya meneja huyo wa Uholanzi kushindwa kutwaa mataji na wachezaji aliokuwa nao.
Hapo ndipo wanahisa wakuu wa klabu hiyo, INEOS, wakamleta Amorim kumrithi wakinuia kubadilisha taswira huko Old Trafford.
Mtaalamu huyo wa Ureno, ambaye alipata kulinganishwa na Jose Mourinho baada ya kuiongoza Sporting CP kutwaa mataji mawili ya Liga ya Ureno, aliwasili Manchester huku akiwa na matarajio ya kuandikisha msururu wa matokeo chanya katika msimu wake wa kwanza.
Hata hivyo, hali haijakuwa hali Old Trafford na msisimko aliowasili nao Amorim ulififia haraka, huku Mreno huyo akishindwa kuthibiti meli kwenye dhoruba kali ya matokeo yasiyoridhisha.
Kipigo cha The Red Devils dhidi ya Tottenham Hotspur Jumapili kilikuwa cha 12 katika Ligi ya Premia msimu huu.
Mara ya mwisho walipoteza hivyo mara nyingi katika mechi 25 za kwanza za msimu mmoja ilikuwa 1973/74 - kampeni ambayo walishuka daraja.
Fomu hii imesababisha maswali mengi juu ya uwezo wa Amorim kuongoza wababe hao wa Mancunian na ripoti kutoka Uhispania sasa imedokeza kwamba mustakabali wake Old Trafford haujulikani.
Kulingana na Fichajes, United tayari wanafikiria juu ya "uingizwaji mpya" kufuatia kushindwa kwa Amorim kuweka kitambulisho wazi na kutoa matokeo mazuri kwa msingi thabiti.
INEOS wameamua kumweka usukani mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 40 hadi mwisho wa msimu isipokuwa “kutokea maafa ambayo yanalazimisha hatua kali kuchukuliwa kabla ya wakati.”
Hata hivyo, inadaiwa bodi ya United tayari imeanza "kutathmini njia mbadala" za nafasi yao ya usimamizi kabla ya dirisha la usajili la majira ya kiangazi.
Vyombo vya habari vya Uhispania vinapendekeza kwamba timu ya Ligi ya Premia wanataka kupata meneja ambaye anaweza kuwageuza kuwa wapinzani wakubwa barani Ulaya.
Ipasavyo, mastaa kama Zinedine Zidane, Thomas Tuchel, na Mauricio Pochettino wanaweza kuwa kwenye orodha ya wagombea.
INEOS alichukua muda mfupi kuachana na Dan Ashworth baada ya kukaa miezi kadhaa akimwinda mkurugenzi wa zamani wa michezo wa Newcastle United.
Kwa hivyo, si jambo la kufikirika kusema wanaweza kumvuta Amorim mapema kuliko ilivyotarajiwa iwapo mambo hayataimarika uwanjani.