Bondia wa Nigeria, Gabriel Oluwasegun Olanrewaju, ameaga dunia baada ya kuzimia ulingoni wakati wa pambano la uzani wa light heavyweight nchini Ghana mnamo Machi 29, 2025.
Bondia huyo mwenye uzoefu, ambaye alikuwa bingwa wa kitaifa na wa Afrika Magharibi, alipoteza fahamu katika raundi ya tatu ya pambano lake dhidi ya mpinzani wake kutoka Ghana, Jon Mbanugu.
Pambano hilo lilikuwa sehemu ya Ligi ya Ngumi ya Kitaalamu ya Ghana na lilifanyika katika Ukumbi mashuhuri wa Bukom Boxing Arena mjini Accra.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Ngumi ya Ghana (GBA), wahudumu wa afya walimpa huduma ya kwanza kabla ya kumkimbiza katika Hospitali ya Mafunzo ya Korle-Bu. Licha ya juhudi zao, alitangazwa kufariki dakika 30 baada ya kufikishwa hospitalini.
Akizungumzia msiba huo, Katibu Mkuu wa Bodi ya Kudhibiti Ngumi ya Nigeria, Remi Aboderin, alimsifu Oluwasegun kwa ujasiri wake na moyo wake wa kupigana.
"Tumepokea taarifa hii kwa masikitiko makubwa," Aboderin aliambia BBC Sport Africa. "Alikuwa mpiganaji asiyeogopa, shujaa halisi ulingoni. Hatukuwahi kutarajia hili, lakini tutatimiza wajibu wetu kwa kusimama imara na familia yake katika kipindi hiki kigumu."
Kabla ya pambano lake la mwisho dhidi ya Mbanugu, Oluwasegun alikuwa na rekodi rasmi ya mapambano 23 ya kulipwa, akishinda 13 na kupoteza nane.
Kifo chake, ambacho kimetokea siku chache zilizopita, ni pigo kubwa kwa jamii ya ngumi nchini Nigeria na Afrika Magharibi kwa ujumla.