
Vigogo wa soka nchini Gor Mahia wameongeza matumaini yao ya kushinda taji lao la 21 la Ligi Kuu ya Kenya baada ya kuwalaza KCB 1-0 katika uwanja wa Kenyatta mjini Machakos mnamo Jumatatu.
Bao la nahodha Austin Odhiambo dakika ya 33 liliipa K'Ogalo ushindi huo muhimu. Mechi hiyo ambayo awali ilipangwa kuchezwa Jumapili, iliahirishwa hadi Jumatatu kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha uwanja kujaa maji.
Kocha mkuu wa Gor Mahia Sinisa Mihic aliwamwagia sifa wachezaji wake akisema walionyesha ustadi wa hali ya juu wa kimichezo na kudhihirisha umahiri wao katika mechi iliyokuwa na ushindani mkubwa.
"Nimefurahishwa na jinsi tulivyocheza kwenye mechi. Wapinzani wetu wana wachezaji wengi wenye vipaji na uzoefu, jambo ambalo lilifanya kuwa mechi ngumu," Mihic alisema.
Ushindi huo umewaacha vinara hao katika nafasi ya tatu kwenye jedwali, wakiwa wamejikusanyia pointi 46 hadi sasa baada ya mechi 25.
Kenya Police wako kileleni mwa jedwali kwa alama 49 wakifuatiwa kwa karibu na watengenezaji divai Tusker ambao wamejikusanyia alama 48.