
BARCELONA, UHISPANIA, Julai 24, 2025 — Mshambuliaji wa kimataifa wa Uingereza, Marcus Rashford, ametambulishwa rasmi kama mchezaji mpya wa FC Barcelona baada ya kukamilisha uhamisho wa mkopo wa msimu mmoja kutoka Manchester United.
Katika hatua hiyo, Rashford amechagua kuvaa jezi nambari 14 — nambari ambayo imewahi kuvaliwa na magwiji waliotamba katika historia ya klabu hiyo.
Akizungumza na wanahabari katika hafla ya utambulisho wake iliyofanyika kwenye Uwanja wa Estadi Olímpic Lluís Companys, Rashford alisema amepata heshima kubwa kujiunga na klabu ya Barcelona, akiahidi kutoa mchango wake kikamilifu.

“Ni heshima kubwa kwangu kuwa sehemu ya klabu yenye historia na mafanikio makubwa barani Ulaya. Najivunia kuvalia jezi hii na nipo tayari kwa changamoto mpya,” alisema Rashford.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27, ambaye anatarajiwa kuongeza makali katika safu ya ushambuliaji ya Barcelona, alieleza kuwa anafahamu uzito wa kuvaa jezi nambari 14.
“Najua nambari hii imewahi kuvaliwa na wachezaji wakubwa kama Johan Cruyff na Thierry Henry. Nitajitahidi kwa kila njia kuendeleza heshima ya nambari hiyo,” aliongeza.

Mkurugenzi wa michezo wa Barcelona, Deco, alieleza matumaini ya klabu hiyo kwa usajili wa Rashford, akisema kuwa mchezaji huyo ataleta uzoefu wa kimataifa unaohitajika kwenye kikosi hicho.
“Marcus ni mchezaji aliyekamilika. Ana uzoefu wa Ligi Kuu ya Uingereza na mashindano ya kimataifa. Atakuwa msaada mkubwa kwa benchi la ufundi na kikosi kwa ujumla,” alisema Deco.
Kwa upande wa Manchester United, kocha mkuu Ruben Amorim alimtakia mchezaji huyo kila la heri katika changamoto yake mpya.
“Marcus anahitaji mazingira mapya ya kujenga upya kiwango chake. Tuna imani ataweza kurejea kwa kiwango bora zaidi,” alisema Amorim.

Barcelona wanatarajiwa kuanza msimu wao mpya wa La Liga mwezi ujao, huku Rashford akipewa nafasi kubwa ya kushirikiana na nyota wengine kama Robert Lewandowski na Lamine Yamal katika safu ya ushambuliaji.
Uhamisho huo wa mkopo hauna kipengele cha ulazima wa kununuliwa, lakini taarifa zinaeleza kuwa iwapo Rashford atang'ara, mazungumzo ya uhamisho wa kudumu huenda yakafufuliwa.