Kenya yaongoza mataifa ya Afrika katika jedwali la medali licha ya matokeo hafifu kwenye Olimpiki

Licha ya msururu wa matokeo hafifu ambayo Kenya imeandikisha, ushindi wa jana katika mbio za mita 800 ulisukuma Kenya katika nafasi bora miongoni mwa mataifa ya bara Afrika.

Muhtasari

•Kwa sasa nchi ya Kenya imeshikilia nafasi ya 38 kote duniani kwenye jedwali ya medali ikiwa na medali tano.

•Dhahabu moja ya Kenya ilitwaliwa na Emmanuel Korir huku medali mbili za fedha zilinyakuliwa na Ferguson Rotich na Hellen Obiri. Medali  za shaba zilinyakuliwa na Benjamin Kigen na Hyvin Kiyeng.

Emmanuel Rotich na Ferguson Rotich
Emmanuel Rotich na Ferguson Rotich
Image: HISANI

Ni  dhahiri kuwa mashindano ya Olimpiki yanayoendelea jijini Tokyo, Japan  yameenda kinyume ya matarajio ya Wakenya wengi ambao walikuwa na imani kubwa na timu inayowakilisha taifa.

Licha ya msururu wa matokeo hafifu ambayo Kenya imeandikisha, ushindi wa jana katika mbio za mita 800 ulisukuma Kenya katika nafasi bora miongoni mwa mataifa ya  bara Afrika.

Kwa sasa, siku ya 13 ya mashindano ya Olimpiki nchi ya Kenya imeshikilia nafasi ya 38 kote duniani kwenye jedwali ya medali ikiwa na medali tano.

Medali moja ya dhahabu, mbili za fedha na mbili za shaba zimefanikisha Kenya kuwa kileleni miongoni mwa mataifa ya Afrika huku Afrika Kusini ikifuata kwa karibu na dhahabu moja, fedha mbili. Afrika Kusini imekalia nafasi ya 39 kote duniani.

Ethiopia na Uganda zimeshikilia nafasi ya 3 barani Afrika na nafasi ya 46 kote duniani kwa pamoja. Mataifa hayo mawili yamejinyakulia dhahabu moja, fedha moja na shaba moja.

Nchi ya Tunisia inafunga orodha ya mataifa 5 bora barani Afrika kwa sasa ikiwa imenyakua medali moja ya dhahabu na fedha moja.

Dhahabu moja ya Kenya ilitwaliwa na Emmanuel Korir huku medali mbili za fedha zilinyakuliwa na Ferguson Rotich na Hellen Obiri. Medali  za shaba zilinyakuliwa na Benjamin Kigen na Hyvin Kiyeng.

Siku ya Jumapili, Agosti 8, itakuwa hatima ya mashindano hayo na Kenya itaendelea tu kutumai kuwa haitabanduliwa kutoka nafasi bora barani Afrika.