Kenya yaibuka bora barani Afrika kwenye mashindano ya Olimpiki yaliyotamatika Tokyo

Hatimaye mashindano ya Olimpiki yaliyokuwa yanafanyika jijini Tokyo, Japan yalitamatika siku ya Jumapili baada ya siku 17

Muhtasari

•Ushindani mkali ulishuhudiwa kwenye mashindano hayo huku Marekani ikiibuka mshindi  baada ya kunyakua medali 113

•Kenya iliweza kuondoka pale na medali 10; nne zikiwa za dhahabu, nne za fedha na mbilli za shaba

Eliud Kipchoge baada ya kushinda dhahabu usiku wa kuamkia Jumapili
Eliud Kipchoge baada ya kushinda dhahabu usiku wa kuamkia Jumapili
Image: HISANI

Hatimaye mashindano ya Olimpiki yaliyokuwa yanafanyika jijini Tokyo, Japan yalitamatika siku ya Jumapili baada ya siku 17.

Ushindani mkali ulishuhudiwa kwenye mashindano hayo huku Marekani ikiibuka mshindi  baada ya kunyakua medali 113. China na Japan zilishikilia nafasi ya pili na ya tatu zikijinyakulia medali 88 na 58 mtawalia. 

Hata hivyo mataifa ya bara Afrika yalishindwa kung'aa kwenye mashindano hayo huku ushindi wa Eliud Kipchoge usiku wa kuamkia Jumapili ukisukuma Kenya katika nafasi ya 19 kote duniani na kileleni miongoni mwa mataifa ya bara Afrika.

Kenya iliweza kuondoka pale na medali 10; nne zikiwa za dhahabu, nne za fedha na mbilli za shaba. Nchi jirani ya Uganda ilishikilia nafasi ya 35 kote duniani na kuibuka wa pili barani Afrika baada ya kujinyakulia dhahabu mbili, fedha moja na medali moja ya shaba.

Afrika Kusini ilishikilia nafasi ya tatu barani ikienda nyumbani na dhahabu moja na fedha mbili. Taifa la Misri lilijinyakulia dhahabu moja, fedha moja  na nishani nne za shaba. Ethiopia ilifunga orodha ya tano bora barani Afrika na nishani moja ya dhahabu, fedha moja na shaba mbili.

Medali nne za dhahabu ambazo  Kenya ilinyakua zilitwaliwa na Emmanuel Korir, Peres Jepchirchir, Faith Kipyegon na Eliud Kipchoge.

 Ferguson Rotich, Brigid Kosgei, Timothy Cheruiyot  na Hellen Obiri walinyakulia Kenya nishani za fedha huku  Benjamin Kigen na Hyvin Kiyeng wakishinda shaba.