Mwanariadha wa mita mia moja Fernidand Omanyala ni mtu mwenye furaha baada ya kuingia katika mkataba wa mamilioni ya pesa na kampuni ya Adidas.
Kampuni hiyo ya Kijerumani inajulikana kwa kutengeneza bidhaa za spoti zikiwemo jezi,viatu, mipira miongoni mwa zingine nyingi.
Katika mkataba huo unaotajwa kuwa wa miaka mitatu, Omanyala pia atakuwa anafaidi ada za kusafiri, mavazi ya spoti pamoja na marupurupu mengine iwapo ataibuka mshindi katika mashindano mbali mbali.
Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio nchini, Omanyala alifichua kuwa katika mkataba huo na kampuni ya Adidas, pia kuna kipengele cha kuurefusha mkataba kwa mwaka mmoja zaidi iwapo atazidi kufana katika mbio za mita mia moja.
"Ni pesa nzuri na pia watasimamia ada ya usafiri, mavazi ya spoti na marupurupu katika kila ushindi ambao nitakuwa napata. Mwaka huu ninalenga kuvunja na pia kuandikisha rekodi mpya katika mbio za mita 100, tofauti na mwaka jana," Omanyala alisema.
Mwanariadha huyo pia aliongeza kuwa ana nia ya kujitosa katika mbio za mita 200 ila akasisitiza kuwa uamuzi huo utamuhitaji kutenga muda zaidi kwa ajili ya mazoezi kwa sababu mbio hizo ni tofauti na zile za mita 100 ambazo ndicho kitengo chake rasmi.
Nyota ya Omanyala, 25, ilianza kung'aa mwaka jana baada ya kutia fora katika mashindano ya Olimpiki huko Tokyo nchini Japan, mashindano ambayo aliibuka wa nne.
Baadae mwishoni mwa mwaka jana, mwanariadha huyo alizidi kung'ara katika mashindano mbali mbali, matukio ambayo yalimpa umaarufu mkubwa miongoni mwa wakenya, taasisi za serikali pamoja na makampuni ya ubashiri nchini.