Mwanariadha wa masafa marefu Franklin Chepkwony azirai na kufariki baada ya zoezi

Chepkwony alijipata katika midomo ya wapenzi wa riadha mwaka 2012 alikoshiriki riadha za masafa marefu mjini Zurich na kumaliza wa kwanza kwa muda wa 2:10:57.

Muhtasari

•  Mwaka 2014, Chepkwony alishiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano ya mbio za dunia na kumaliza wa tatu katika mbio za Boston nchini Marekani.

Franklin Chepkwony
Franklin Chepkwony
Image: Maktaba

Wapenzi wa mchezo wa riadha za masafa marefu humu nchini wametupwa katika kipindi cha maombolezo baada ya mwanariadha wa masafa marefu Franklin Chepkwony kuanguka, kuzirai na kufariki baada ya mazoezi.

Chepkwony ni mshindi wa mbio za masafa marefu za Seoul, Korea Kusini mwaka 2013 na alifariki Jumatatu asubuhi kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Daily Nation.

Inaarifiwa alizirai na kufariki akiwa njiani kutoka mazoezini katika eneo la Eldama Ravine kaunti ya Baringo.

Chepkwony alijipata katika midomo ya wapenzi wa riadha mwaka 2012 alikoshiriki riadha za masafa marefu mjini Zurich na kumaliza wa kwanza kwa muda wa 2:10:57.

Kisha alishiriki pia mashidnano ya masafa marefu mjini Eindhoven nchini Uholanzi na kumaliza wa pili kwa muda wa 2:06:11 mwaka huo huo.

Alirejea ulingoni mwaka mmoja baadae na kushiriki mbio za Seoul nchini Korea Kusin alikoshinda kwa muda wa 2:06:59.

 Mwaka 2014, Chepkwony alishiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano ya mbio za dunia na kumaliza wa tatu katika mbio za Boston nchini Marekani.

 Rafiki yake ambaye walikuwa wanafanya zoezi naye alisema kuwa walikuwa wamejiratibia kushiriki mazoezi ya kilomita 23 asubuhi hiyo ya Jumatatu na walikuwa wameshiriki mazoezi ya kupasha misuli moto.

Familia yake iliambia gazeti la Nation kwamba tayari wameanzisha mipango ya kumpa heshima za mwisho, huku mwili wake ukiwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Eldama Ravin.