Mwanariadha Lawrence Cherono akabiliwa na mashtaka ya utumizi wa dawa za kusisimua misuli

Bingwa huyo wa Chicago Marathon 2019 amejikuta katika upande mbaya na kitengo cha uadilifu cha riadha kutokana na utumizi wa dawa ya kusisimua misuli.

Muhtasari

•Mwanariadha Lawrence Cherono anakabiliwa na mashtaka ya utumizi wa dawa aina ya trimetazidine,inayofahamika kusisimua misuli.

• Hii ni mara ya pili kwa mwanariadha huyo baada ya kupigwa marufuku Julai,2022

Lawrence Cherono
Image: Hisani

Lawrence Cherono ambaye ni bingwa  wa Chicago Marathon 2019 ,ameshtakiwa kwa utumizi wa dawa za kusisimua misuli na kitengo cha uadilifu cha riadha (AIU).

Katika taarifa kupitia ukurasa wa X  Jumatano 12,Juni 2024, shirika la kupambana na dawa za kusisimua misuli lilithibitisha kuwa bingwa huyo mara mbili wa Amsterdam Marathon ameshtakiwa kwa utumizi wa dawa ya kusisimua misuli.

Hii si mara ya kwanza kwa mwanariadha huyo kwani,Julai 2022, Cherono alipigwa marufuku kwa muda baada ya kupimwa kuwa na dawa inayofahamika kama trimetazidine.

Dawa hii inajulikana kuboresha matumizi ya moyo ya oksijeni, uwezekano wa kuwapa wanariadha faida isiyo ya haki kwa kuimarisha viwango vyao vya uvumilivu.

Cherono alikuwa ameratibiwa kuwakilisha Kenya katika mashindano ya dunia huko Oregon, pamoja na Geoffrey Kamworor na Barnabas Kiptum, ndoto ambayo kwa sasa imesitishwa.

Mwanariadha huyo alishiriki mbio zake za mwisho kule Boston Marathon mnamo Aprili 2022 ambapo alitumia muda wa takriban 2:07:21  akimaliza kwa nafasi ya pili.