Olimpiki ya Paris: Orodha ya wanariadha ambao wameshindia Kenya medali zote 11

Timu ya Kenya imeleta nyumbani dhahabu nne, fedha mbili, na shaba tano kutoka Olimpiki ya Paris.

Muhtasari

• Obiri aliibuka wa  tatu katika mbio za marathon ya wanawake za na kuishindia Kenya medali ya 11  katika mashindano Paris Olympics.

•Medali za dhahabu zilinyakuliwa na Beatrice Chebet, Faith Kipyegon na Emmanuel Wanyonyi.

walishindia Kenya dhahabu na fedha katika mbio za mita 5000 kwa wanawake.
Faith Kipyegon na Beatrice Chebet walishindia Kenya dhahabu na fedha katika mbio za mita 5000 kwa wanawake.
Image: HISANI

Mwanariadha wa Kenya wa mbio za marathon Hellen Obiri aliibuka nambari tatu katika mbio za marathon ya wanawake za Olimpiki za Paris mnamo Jumapili asubuhi na kuipa Kenya medali ya kumi na moja katika mashindano hayo.

Obiri alikamilisha mbio hizo za kilomita 42 kwa muda wa saa 2.23.10, nyuma ya Sifan Hassan wa Uholanzi (2.22.55) na Tigist Asefa wa Ethiopia (2.22.58).

Mkenya mwingine, Sharon Lokedi aliibuka wa nne baada ya kukimbia kwa saa 2.2314, akikosa medali kwa sekunde chache tu.

Obiri na Lokedi walipambana vikali na walikuwa wakiongoza pamoja kwa muda mrefu katika kilomita za mwisho za mbio hizo kabla ya Hassan na Asefa kuwazidi nguvu katika takriban mita mia mbili za mwisho.

Shaba katika mbio za marathon za wanawake sasa inafikisha jumla ya medali za shaba zilizoshindwa na Wakenya katika Michezo ya Olimpiki ya Paris hadi tano.

Timu ya Kenya pia imeleta nyumbani dhahabu nne, na fedha mbili.

Medali za dhahabu zilinyakuliwa na Beatrice Chebet katika mbio za mita 5000 na 10000 kwa wanawake, Faith Kipyegon katika mbio za mita 1500 kwa wanawake, na Emmanuel Wanyonyi katika mbio za mita 800 kwa wanaume.

Faith Kipyegon pia alishinda nchi hiyo medali ya fedha katika mbio za mita 5000 kwa wanawake huku Ronald Kwemoi akishinda medali hiyo katika mbio za mita 5000 kwa wanaume.

Mary Moraa (mbio za mita 800 za wanawake), Faith Cherotich (mbio za mita 3000 kwa wanawake kuruka viunzi), Abraham Kibiwot (mbio za mita 3000 kuruka viunzi wanaume), Benson Kipruto (Mbio za Marathon za Wanaume), na Hellen Obiri aliyeibuka wa tatu katika mbio za wanawake marathon waliletea Kenya medali za shaba.