
Mchezo wa mwisho wa derbi ya Merseyside katika uwanja wa
Goodison Park ulihitimishwa kwa vurugu baada ya Everton na Liverpool kutoka
sare ya 2-2, huku wachezaji wawili, kocha wa Liverpool na msaidizi wake wakitolewa
nje kwa kadi nyekundu.
Curtis Jones wa Liverpool, Abdoulaye Doucouré wa Everton, kocha Arne Slot , pamoja na msaidizi wake, walifukuzwa uwanjani kufuatia ghasia zilizotokea mwishoni mwa mchezo huo wa kusisimua.
Everton walifungua ukurasa wa mabao mapema kupitia kwa mshambuliaji wao, Beto, kabla ya Alexis Mac Allister wa Liverpool kusawazisha.
Mohamed Salah aliiweka Liverpool kifua mbele, lakini James Tarkowski aliisawazishia Everton katika dakika ya 98 kwa shuti kali kutoka kwa kona.
Baada ya filimbi ya mwisho, hali ilibadilika ghafla kutoka shangwe hadi vurugu. Mabishano makali kati ya wachezaji wa timu zote mbili yalipelekea ugomvi, na mwamuzi hakuwa na budi ila kuchukua hatua kali.
Curtis Jones alipata kadi nyekundu kutokana na kushiriki katika ugomvi na baadhi ya wachezaji wa Everton, kitendo kilichoonekana kuwa cha uchokozi. Kwa upande mwingine, Abdoulaye Doucouré wa Everton naye hakusalia nyuma, akijibu kwa hasira, jambo lililomlazimu mwamuzi kutoa kadi nyekundu dhidi yake pia.
Kocha wa Liverpool, Arne Slot, pamoja na msaidizi wake, walijikuta matatani baada ya kuingia katika majibizano makali na benchi la Everton na waamuzi wa mechi. Katika hali hiyo ya taharuki, mwamuzi aliamua kuwapa adhabu ya kadi nyekundu kwa tabia yao ya utovu wa nidhamu.
Mchezo huu ulikuwa wa mwisho wa derbi ya Merseyside kufanyika
Goodison Park kabla ya Everton kuhamia uwanja wao mpya. Licha ya vurugu
zilizoshuhudiwa, mechi hii itaendelea kukumbukwa kwa ushindani mkubwa na mabao
ya dakika za mwisho.
Liverpool sasa inasubiri hatma ya rufaa au adhabu zaidi kutoka kwa FA kuhusu kadi hizo nyekundu, huku Everton wakihesabu hasara ya kumkosa Doucouré katika mechi zijazo.