logo

NOW ON AIR

Listen in Live

"Mchezo Mbaya Zaidi!" Kocha Maresca Avunjwa Moyo Na Chelsea Kufuatia Kipigo Cha 3-0 Kutoka Kwa Brighton

Maresca alieleza wazi kusikitishwa na kiwango cha timu yake, akisema wachezaji wake walikosa hamasa ya kupambana.

image
na Samuel Mainajournalist

Football15 February 2025 - 09:45

Muhtasari


  • Maresca, amekosoa ari ya wachezaji wake baada ya kipigo kizito cha 3-0 kutoka kwa Brighton, akikitaja kama "mchezo mbaya zaidi"
  •  Maresca alisema kuwa tatizo kubwa halikuwa uwezo wa kumiliki mpira, bali ukosefu wa ari ya ushindani.

Enzo Maresca

Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, amekosoa ari ya wachezaji wake baada ya kipigo kizito cha 3-0 kutoka kwa Brighton, akikitaja kama "mchezo mbaya zaidi" tangu ajiunge na klabu hiyo.

 Katika kipindi cha siku sita pekee, Chelsea imeshindwa mara mbili dhidi ya Brighton, kwanza ikitolewa kwenye Kombe la FA, na sasa ikipokea pigo lingine kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.

 Mabao kutoka kwa Kaoru Mitoma na Yankuba Minteh (mawili) yaliizamisha Chelsea, huku mashabiki waliokuwa wamsafiri wakielezea hasira zao kwa kuimba "Tunataka Chelsea yetu ya zamani."

 Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mechi, Maresca alieleza wazi kusikitishwa na kiwango cha timu yake, akisema wachezaji wake walikosa hamasa ya kupambana.

 "Mashabiki wana haki ya kuwa na hasira, hasa katika kipindi hiki cha msimu ambapo tulikuwa na nafasi ya kusogea karibu na nafasi za juu," alisema Maresca.

 "Tungepata ushindi, tungekuwa pointi moja tu kutoka nafasi ya tatu na kuongeza pengo dhidi ya walioko nyuma yetu."

 Maresca aliongeza kuwa tatizo kubwa halikuwa uwezo wa kumiliki mpira, bali ukosefu wa ari ya ushindani:

 "Tulipaswa kuonyesha zaidi nje ya kumiliki mpira. Leo, huu ulikuwa mchezo mbaya zaidi tangu nifike hapa,” alisema.

 Licha ya Chelsea kuwa na umiliki mkubwa wa mpira, walishindwa kutengeneza nafasi za wazi. Brighton waliongoza mapema kupitia goli la Mitoma, ambaye alitumia vyema pasi ya kipa Bart Verbruggen, kisha Minteh akafunga mabao mawili zaidi, la pili likija muda mfupi baada ya bao la Enzo Fernandez kufutwa kwa faulo dhidi ya Joel Veltman.

 Chelsea, ambayo imekosa mshambuliaji wake namba moja Nicolas Jackson kutokana na jeraha, ilionekana kupoteza mwelekeo mbele ya goli, hali ambayo Maresca alikiri kuwa tatizo kubwa.

 "Tumekuwa tukitengeneza nafasi nyingi, lakini kwa sasa tunaonekana kuruhusu mabao kirahisi huku tukishindwa kufunga. Hilo ni jambo tunalopaswa kulifanyia kazi haraka," alisema.

 Kipigo hicho kiliongezewa machungu na jeraha la Noni Madueke, ambaye alitolewa nje baada ya dakika 21 tu kutokana na jeraha la msuli wa paja (hamstring). Maresca alithibitisha kuwa atakuwa nje kwa muda.

 Kwa upande wa Brighton, ushindi huu uliwapeleka hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi, huku kocha wao Fabian Hurzeler akisifia goli la Mitoma kama "muda wa kipekee."

 Kwa Chelsea, presha ya kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa inaendelea kuongezeka, huku Maresca akikiri kuwa timu yake ina changamoto kubwa kwa sasa.

 "Tuna mechi 13 zilizobaki, tunapaswa kuzimaliza kwa njia bora zaidi," alihitimisha.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved