
Kiungo mshambuliaji wa Chelsea, Cole Palmer, ametajwa kuwa
Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Uingereza mwaka 2025 katika London Football
Awards.
Mbali na tuzo hiyo, staa huyo mwenye umri wa miaka 22 pia amejishindia tuzo la bao bora la msimu kutokana na mkwaju wake wa mpira wa adhabu katika ushindi wa 4-2 dhidi ya Brighton mnamo Septemba mwaka jana.
Katika mchuano huo, Palmer aliweka historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza wa EPL kufunga mabao manne katika kipindi cha kwanza cha mechi.
Katika kinyang’anyiro cha Mchezaji Bora wa Mwaka, Palmer aliwashinda wachezaji kadhaa akiwemo Gabriel Magalhães wa Arsenal, Bryan Mbeumo na Mikkel Damsgaard wa Brentford, pamoja na Antonee Robinson wa Fulham.
Mlinda mlango wa Arsenal, David Raya, alituzwa Kipa Bora wa Mwaka baada ya kuonyesha kiwango cha juu msimu huu, akifanikiwa kuweka clean sheet tisa katika mechi za EPL kufikia sasa.
Tuzo hii inadhihirisha mchango wake mkubwa katika safu ya ulinzi ya Arsenal tangu alipojiunga na timu hiyo mwaka 2023.
Katika vipengele vingine vya tuzo hizo zilizofanyika Wembley Stadium, wachezaji na makocha kadhaa walitambuliwa kwa mafanikio yao msimu huu:
Meneja Bora wa Mwaka: Sonia Bompastor wa Chelsea Women’s, aliyewashinda Mikel Arteta (Arsenal), Andy Woodman (Bromley), Thomas Frank (Brentford) na Richie Wellens (Leyton Orient).
Mchezaji Bora Chipukizi wa Kiume: Archie Gray wa Tottenham Hotspur, aliyewashinda Ethan Nwaneri na Myles Lewis-Skelly (Arsenal), Romain Esse (Crystal Palace), na Rocco Vata (Watford).
Mchezaji Bora wa Wanawake: Guro Reiten wa Chelsea, aliyewashinda Johanna Rytting Kaneryd (Chelsea), Alessia Russo na Frida Maanum (Arsenal), na Beth England (Tottenham).
Mchezaji Bora Chipukizi wa Wanawake: Aggie Beever-Jones wa Chelsea, ambaye ameshinda tuzo hiyo kwa mwaka wa pili mfululizo.
Mchezaji Bora wa EFL: Matty Stevens wa AFC Wimbledon, aliyewashinda Giorgi Chakvetadze (Watford), Jamie Donley (Leyton Orient), Michael Cheek (Bromley), na Japhet Tanganga (Millwall).
Kwa upande mwingine, Sir Gareth Southgate alipewa tuzo ya Power of Football kutokana na mchango wake mkubwa kama kocha wa timu ya taifa ya England, huku Chris Ramsey akitunukiwa Outstanding Contribution Award kwa juhudi zake katika maendeleo ya soka na utofauti wa michezo. Brentford Community Sports Trust ilishinda Community Award kupitia kampeni yao ya Bee a Hero, inayohamasisha uchangiaji damu katika jamii zinazozunguka klabu hiyo.
Tuzo za London Football Awards 2025 zilileta pamoja vipaji bora vya soka jijini London, huku Cole Palmer na David Raya wakivutia vichwa vya habari kwa mafanikio yao makubwa msimu huu.