logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Lengo letu ni kushinda EPL - Amorim asema baada ya United kubanduliwa nje ya FA

"Lengo ni kushinda Ligi Kuu. Najua tunapoteza mechi, lakini lengo ni kushinda tena Ligi Kuu," Amorim alisema.

image
na Samuel Mainajournalist

Football03 March 2025 - 07:18

Muhtasari


  • Amorim anaamini kuwa licha ya changamoto zinazoikumba timu yake kwa sasa, malengo yao makubwa hayajabadilika.
  • United walitolewa kwenye Kombe la FA kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Fulham.

Ruben Amorim

Kocha wa Manchester United, Rúben Amorim, anaamini kuwa licha ya changamoto zinazoikumba timu yake kwa sasa, malengo yao makubwa hayajabadilika—wanataka kushinda Ligi Kuu ya Uingereza.

Kauli hii imezua mjadala mkali, hasa baada ya United kutolewa kwenye Kombe la FA kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Fulham.

Baada ya kipigo hicho cha kusikitisha, Amorim alizungumzia mustakabali wa timu yake na kusisitiza kuwa mafanikio makubwa bado yanawezekana

"Lengo ni kushinda Ligi Kuu. Najua tunapoteza mechi, lakini lengo ni kushinda tena Ligi Kuu. Sijui itachukua muda gani," Amorim aliambia BBC.

Katika mechi hiyo ya mzunguko wa tano wa Kombe la FA, Manchester United ilionyesha mapungufu makubwa.

Fulham walifungua ukurasa wa mabao kupitia Calvin Bassey, huku United wakisawazisha kupitia nahodha wao, Bruno Fernandes.

Mchuano ulienda hadi muda wa ziada, lakini hakuna timu iliyoweza kupata bao la ushindi. Hatimaye, kwenye mikwaju ya penalti, Fulham waliibuka kidedea kwa ushindi wa 4-3 baada ya kipa wao, Bernd Leno, kuokoa penalti muhimu kutoka kwa Victor Lindelöf na Joshua Zirkzee.

Kipigo hicho kiliongeza shinikizo kwa Amorim, ambaye tayari anakabiliwa na changamoto ya kuboresha hali ya United kwenye Ligi Kuu.

Timu hiyo kwa sasa inashikilia nafasi ya 14, ikiwa na tofauti ndogo na timu zilizo kwenye vita vya kushuka daraja.

Baada ya Amorim kusema kuwa Manchester United inalenga kushinda taji la Ligi Kuu, mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Wayne Rooney, hakusita kumkosoa. "Hii ni kauli ya kijinga. United wanapaswa kwanza kurekebisha hali yao mbaya kabla ya kufikiria kuhusu kushinda ligi," alisema Rooney.

Amorim, hata hivyo, hakukaa kimya. "Siko na unyonge. Ndiyo maana niko hapa nikiwa na umri wa miaka 40, nikifundisha Manchester United," alijibu kocha huyo, akisisitiza kuwa ana maono makubwa kwa klabu hiyo licha ya changamoto wanazopitia kwa sasa.

Kama Amorim anavyosema, Manchester United bado wanaweza kufanikisha malengo yao, lakini ukweli ni kwamba wanahitaji kubadilika haraka.

Timu imekuwa na matokeo yasiyoridhisha, na iwapo hawatapata suluhisho, huenda badala ya kupigania ubingwa, watakuwa wakihangaika kuepuka kushuka daraja. 

Mashabiki wa United wanatarajia kuona mabadiliko chanya ili kurejesha hadhi ya klabu yao.

Amorim ana kazi ngumu mbele yake, lakini ikiwa kweli ana ndoto ya kushinda Ligi Kuu, atalazimika kubadili hali ya mambo kwa kasi.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved