
Kipa wa FC Barcelona, Marc-André ter Stegen, ameibuka hadharani kukemea vikali kituo cha redio cha Catalunya Radio na kampuni ya 3Cat Group kwa kusambaza taarifa za uongo kuhusu sababu ya kutengana kwake na mkewe wa zamani, Daniela Jehle.
Katika taarifa rasmi aliyotoa siku ya Jumatatu, Machi 10, Ter Stegen alikanusha madai kuwa ndoa yake ilivunjika kutokana na usaliti wa Daniela, akiwashutumu waandishi wa habari Juliana Canet, Roger Carandell na Marta Montaner kwa kueneza uvumi usio na msingi.
"Nimeshtushwa na kusikitishwa na usimamizi mbovu na ukosefu wa uongozi katika Catalunya Radio na 3Cat Group – vyombo vinavyosambaza habari za uongo na kukiuka haki za kibinafsi," aliandika kipa huyo.
Kwa mujibu wa taarifa yake, Ter Stegen alisisitiza kuwa hakukuwa na usaliti wowote katika ndoa yake, wala mtu wa tatu aliyehusika katika uamuzi wao wa kutengana.
"Hakujawa na usaliti wowote kutoka kwa Daniela. Hakuna mtu mwingine aliyehusika. Huu ni ukweli," alisisitiza.
Hata hivyo, alieleza kuwa yeye na Daniela walifikia makubaliano ya kutengana kwa hali ya amani na maelewano mazuri, wakibaki na mawasiliano yenye heshima.
Kipa huyo raia wa Ujerumani alionyesha ghadhabu kwa jinsi taarifa za uongo zilivyomchafulia mke wake wa zamani hadharani, akielezea kusikitishwa kwake na ukweli kuwa chombo kikuu cha habari kinachomilikiwa na serikali kimekuwa sehemu ya kusambaza uvumi huo.
"Ni jambo lisilokubalika hata kidogo kwa shirika kubwa la habari linalomilikiwa na serikali kusambaza habari hizi zisizo na msingi, ambapo Daniela anatuhumiwa kwa uwongo na kushambuliwa binafsi," aliongeza.
Mlinda lango huyo alihitimisha
kwa kusema kuwa uharibifu uliosababishwa na uvumi huo hauwezi kurekebishwa.
"Madhara yaliyosababishwa hayawezi kurekebishwa. Asanteni," alisema.
Ter Stegen na Daniela walikuwa kwenye mahusiano kwa muda mrefu kabla ya kuoana mnamo mwaka wa 2017.
Daniela, ambaye ni
mbunifu wa usanifu wa majengo, alikuwa akiishi pamoja na kipa huyo jijini
Barcelona, na mara kwa mara walionekana pamoja kwenye matukio ya kijamii na
mechi muhimu za Blaugrana.
Hata hivyo, mnamo Februari 2024, ripoti zilianza kuibuka kuhusu uwezekano wa wawili hao kutengana. Hatimaye, mwezi Machi, Ter Stegen alithibitisha rasmi kuwa ndoa yao ilikuwa imevunjika, ingawa alisisitiza kuwa walitengana kwa amani.
"Baada ya
tafakari ya kina, Daniela na mimi tumeamua kuchukua njia tofauti. Kama
mnavyoweza kudhani, huu haukuwa uamuzi rahisi, lakini tunaamini ni hatua bora
kwetu,"Ter Stegen alisema wiki
jana.
Aliongeza kuwa lengo lao kuu ni kuhakikisha ustawi na mazingira thabiti kwa watoto wao wawili, na kwamba wataendelea kushirikiana kama wazazi huku wakiheshimiana na kuthaminiana kama ilivyokuwa daima.
Kwa sasa, Ter
Stegen anaendelea kuwa nguzo muhimu kwa FC Barcelona, huku uvumi kuhusu maisha
yake ya kibinafsi ukiwa gumzo kubwa katika vyombo vya habari vya Uhispania.