
Mtangazaji
maarufu wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi Radio Jambo, Joseph Ogidi
almaarufu Gidi Ogidi, ametangaza kujiondoa rasmi kwenye kinyang’anyiro cha
nafasi ya Katibu Mkuu wa klabu ya soka ya Gor Mahia, siku mbili kabla ya
uchaguzi mkuu wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Jumapili, Aprili 13.
Katika taarifa rasmi kwa vyombo vya habari iliyotolewa Ijumaa, Ogidi amesema kuwa uamuzi huo haukuwa mwepesi, lakini amelazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na "mazingira yaliyo nje ya uwezo wake."
Huku akionyesha heshima kwa mchakato wa uchaguzi na amri ya mahakama kuhusu uchaguzi huo, Ogidi amesema hatatoa maelezo zaidi hadi baada ya kipindi cha uchaguzi kukamilika.
“Kwa heshima ya mchakato unaoendelea na kwa kuzingatia agizo la mahakama kuhusu uchaguzi uliopangwa, sitatoa maelezo ya kina kuhusu sababu za kujiondoa kwangu hadi uchaguzi utakapotamatika,” alisema Gidi.
Mwimbaji huyo wa zamani ambaye ni shabiki sugu na mwanachama wa muda mrefu wa Gor Mahia, alitangaza azma yake ya kuwania nafasi hiyo mapema mwezi huu kupitia ujumbe uliosambaa mitandaoni, akiahidi uongozi wa uwazi, ufanisi, na jumuishi.
Wakati akitangaza azma yake, alisisitiza kuwa ana nia ya kuliletea klabu mabadiliko chanya na kulijenga upya kwa misingi ya uwajibikaji.
Hata hivyo, katika taarifa yake ya kujiondoa, alieleza kuwa dhamira yake kwa Gor Mahia na mashabiki wake bado haijatetereka.
“Naamini katika umoja, uwazi na uongozi wa uadilifu, na ndiyo sababu nimeamua kutoruhusu hali zangu binafsi kuwa kikwazo kwa mchakato huu muhimu,” aliongeza.
Gidi pia alitoa shukrani kwa wote waliomuunga mkono katika safari yake ya kisiasa ndani ya klabu, akiahidi kuendelea kulitumikia Gor Mahia kwa namna yoyote ile atakayoweza siku za usoni.
Kwa sasa, hatua ya kujiondoa kwake imeibua maoni tofauti miongoni mwa wanachama wa klabu hiyo, huku baadhi wakisikitishwa na uamuzi huo, lakini wakimtakia kila la heri katika juhudi zake za baadaye.
Uchaguzi
wa Gor Mahia umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu kutokana na mvutano wa muda mrefu
wa kiuongozi ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.