
Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, ambaye pia ni shabiki sugu wa klabu ya Gor Mahia, Joseph Ogidi almaarufu GidiGidi, ametangaza rasmi nia yake ya kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa klabu hiyo maarufu.
Katika taarifa aliyotoa jioni ya Jumatatu, mwimbaji huyo wa zamani wa kundi la GidiGidi MajiMaji alieleza kuwa tayari amewasilisha rasmi fomu yake ya kuwania nafasi hiyo.
Alisema kuwa ni heshima kubwa kwake kuwania wadhifa huo, akisisitiza kuwa sapoti yake kubwa na mchango wake kwa ulimwengu wa soka kwa muda mrefu unamfanya kuwa mgombea bora.
“Wanachama wapendwa wa klabu ya Gor Mahia, ni heshima kubwa kwangu kuwasilisha azma yangu ya kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa klabu yetu pendwa,” alisema Gidi kupitia taarifa aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii.
Gidi alieleza kuwa iwapo atapata nafasi hiyo, ataihudumia klabu kwa ari, bidii, na ufanisi mkubwa.
“Kama shabiki wa muda mrefu na mshiriki hai wa jamii yetu ya soka, naleta siyo tu mapenzi ya dhati kwa mchezo huu bali pia dhamira ya uongozi ulio wazi, unaofanya kazi kwa ufanisi na unaojumuisha wote,” aliongeza.
Mara tu baada ya kutangaza nia yake, makumi ya mashabiki na watu mashuhuri kama Jalang’o, Suzanna Owiyo, na The Dee Experience walimpongeza na kumtakia kila la heri kupitia mitandao ya kijamii.
Hii si mara ya kwanza kwa Gidi kuwania nafasi ya uongozi katika Gor Mahia. Mnamo mwaka 2013, aligombea nafasi ya mweka hazina lakini hakufanikiwa.
Gor Mahia, klabu yenye mafanikio makubwa zaidi nchini Kenya, itafanya uchaguzi wake mnamo Aprili 13, 2025, katika Uwanja wa Taifa wa Nyayo, eneo la ukumbi wa mpira wa vikapu, kuanzia saa tatu asubuhi.
Sisi kama familia ya Radio Jambo tunamtakia Gidi kila la heri anapopiga hatua hii muhimu ya kulitumikia klabu analolipenda kwa dhati.