
KATIKA kipindi cha Patanisho kwenye Gidi na Ghost Asubuhi ndani ya Radio Jambo, kijana kwa jina Elias mwenye umri wa miaka 23 kutoka Kisii aliomba kupatanishwa na mkewe Moraa mwenye umri wa miaka 20.
Elias alieleza kwamba mke wake
alimkasirikia na kuenda kwao baada ya mama mkwe kupiga simu akitaka kuzungumza
na mamake, jambo ambalo lilimfanya mkewe kuhisi kwamba alikuwa anasengenywa.
Kijana huyo alieleza kwamba hata hivyo,
mkewe baada ya kufika kwao, mamake alimtaka kurudi katika ndoa yake ili
kuyatatua na familia ya mumewe, na kweli akatii na kurudi japo bado alikuwa na
hasira ndani ya nyumba.
Elias alieleza kwamba mkewe amekuwa na
shida na mamake kiasi kwamba hawazungumzi na hata wakikutana njiani mmoja
anaweza kanyaga mwenzake akipita.
“Tumekaa kwa ndoa kwa mwaka mmoja na
tuko na mtoto mmoja, nilikosana na mke wangu wiki moja iliyopita baada ya
mamake kupiga simu akitaka kuzungumza na mamangu,” Elias alieleza.
“Shida ilikuwa kwamba mke wangu
hazungumzi na mamangu hata akipita njiani anaweza mkanyaga akienda, sasa
mamangu akiniuliza mbona mke wako haniongeleshi na nikikaa na mke wangu
kuzungumza naye nijue shida iko wapi nitatue, haniambii,” aliongeza huku
akisisitiza mamake hajawahi mkosea mke wake.
Elias alisema mkewe alirudi kwa nyumba
lakini hazungumzi naye na hata usiku wa jana hakulala kwa nyumba na baada ya
kurudi asubuhi alimpata mkewe bado amemnunia na alitaka azungumziwe ili aache
kununa.
Kwa bahati mbaya, Moraa alipopigiwa
simu, alisikia sauti ya Elias na alipomtajia suala la mamake, Moraa alikata
simu na kuzima.
Elias alifunguka zaidi kwamba mkewe
amekuwa na hulka ya kumwangalia miguu kila anapolala kazini na kurudi alfajiri.
Kulingana na Elias, yeye hufanya kazi
ya kusafirisha mchanga kwa lori na wakati mwingine hulala kazini kwa gari
wanapochelewa, na pindi anaporudi alfajiri, kitu cha kwanza mkewe anafanya ni
kumkagua miguu.
Mkewe akipata miguu ni safi, anamtuhumu
kwamba alikuwa amelala kwa mwanamke aliyemuosha na akipata miguu ni chafu,
anaridhika kwamba alilala kazini.
“Unajua mke wangu kitu cha kwanza
nikifika kwa nyumba anaangalia miguu. Akipata niko msafi ananiuliza nimelala na
nani. Akipata ni chafu anajua nimetoka kazini,” alisema.
“Akipata ni safi ananiambia rudi kwa
huyo mwenye alikuwa amekuweka vizuri sasa kesi zinakuwa nyingi, sasa hiyo
shinda ndio inakuwa kwa nyumba,” Elias aliongeza.